65. Kufaa kukusanya wakati wa mvua, matope na mafuriko

Swali 65: Unasemaje kuhusu kukusanya kwa ajili ya mvua kati ya Maghrib na ´Ishaa katika wakati wa sasa katika miji na mitaa ya lami iliyothibitishwa imara kukiwa hakuna ugumu wala matope?

Jibu: Hapana neno kukusanya kati ya Maghrib na ´Ishaa wala kati ya Dhuhr na ´Aswr kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni kutokana na mvua inayofanya kuwa vigumu kutoka kwenda misikitini. Vivyo hivyo mafuriko yanayomiminika katika masomo kutokana na ule ugumu unaopatikana katika jambo hilo. Msingi wa hilo ni yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa):

“Ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikusanya Madiynah kati ya Dhuhr na ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa.” Muslim amezidisha katika upokezi wake: “… pasi na khofu, mvua wala safari.”

Hilo likafahamisha kwamba ilithibitika kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) ya kwamba khofu na mvua ni udhuru wa kukusanya kama vile safari. Lakini haifai kufupisha katika hali hii. Kinachofaa ni kukusanya peke yake kwa sababu wao ni wakazi na sio wasafari. Kufupisha ni miongoni mwa ruhusa za safari peke yake.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 70
  • Imechapishwa: 12/09/2022