65. Dalili kwamba matarajio ni ´ibaadah na kwamba kumtegemea Allaah hakupingani na mtu kufanya sababu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya utegemeaji ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Na kwa Allaah pekee tegemeeni ikiwa nyinyi ni waumini!”[1]

وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

“Na yeyote yule atakayemtegemea Allaah, basi Yeye humtosheleza.”[2]

MAELEZO

Utegemezi maana yake ni kuyategemeza mambo kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Huku ndio kutegemea. Ni miongoni mwa aina kubwa za ´ibaadah. Kwa ajili hiyo amesema:

وَعَلَى اللَّـهِ فَتَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Na kwa Allaah pekee tegemeeni ikiwa nyinyi ni waumini!”

Bi maana Kwake pekee na si kwa mwingine. Kisha akasema:

إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“… ikiwa nyinyi ni waumini!”[3]

Amefanya ni miongoni mwa sharti za imani kule kutegemea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni dalili iliyofahamisha kwamba yule asiyemtegemea Allaah sio muumini.

Utegemeaji ni ´ibaadah kubwa. Muumini siku zote ni mwenye kumtegemea Allaah (´Azza wa Jall). Allaah miongoni mwa majina Yake ni al-Wakiyl (mtegemewaji). Ni mwenye kutegemezewa mambo ya waja Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Kutegemea hakukuwi isipokuwa kwa Allaah. Haijuzu mtu kusema kuwa amemtegemea fulani. Kwa sababu utegemeaji ni ´ibaadah na ´ibaadah haiwi isipokuwa kwa Allaah. Ama mtu akimwachia mwengine amsimamie mambo yake kitendo hicho hakiitwi kuwa ni utegemeaji (توكلًا). Kitendo hicho kinaitwa uwakilishaji (توكيلً). Uwakala unatambulika ambapo unamuwakilisha mtu akusimamie haja yako. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwaweka wenye kumkalia niaba yake katika baadhi ya kazi zake. Kwa hiyo uwakala sio utegemeaji. Utegemeaji ni ´ibaadah ambayo hafanyiwi isipokuwa Allaah. Wala haijuzu kwako kusema kwamba umemtegemea fulani. Unachotakiwa kusema ni kwamba umemuwakilisha fulani. Pamoja na haya muwakilishe na wala usitegemee kwake. Bali unatakiwa kutegemea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa hiyo zingatieni tofauti kati ya mambo hayo mawili; utegemeaji na uwakalishaji.

Miongoni mwa sifa za waumini ni zile alizotaja Allaah (Ta´ala) pale aliposema:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللّهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَى رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ

“Hakika si vyenginevyo waumini ni wale ambao anapotajwa Allaah nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayah Zake basi huwazidishia imani na kwa Mola wao wanategemea.”[4]

Hizi ni miongoni mwa sifa za waumini. Utegemeaji ni ´ibaadah tukufu asiyofanyiwa isipokuwa Allaah (´Azza wa Jall) pekee kwamba Yeye ndiye muweza wa kila jambo, mfalme wa kila kitu na kwamba Yeye ndiye muweza wa kukutekelezea mahitajio yako. Kuhusu kiumbe pengine asiweze kukutekelezea mahitajio yako. Ukimuwakilisha akutekelezee kazi fulani lakini hata hivyo mtegemee Allaah katika kufikia jambo hilo.

Jengine linalotakiwa kutambulika ni kwamba kumtegemea Allaah hakupingani na mtu kufanya sababu. Kwa msemo mwingine ni kwamba muislamu anatakiwa kukusanya kati ya kumtegemea Allaah na kufanya sababu na wala mawili hayo hayapingani. Wewe unatakiwa ufanye sababu ulizoamrishwa kufanya lakini usitegemee sababu hizo. Mtegemee Allaah. Kupanda mbegu ardhini ni moja katika sababu. Lakini usitegemee kilimo na kitendo chako. Bali mtegemee Allaah akikuze kilimo hicho, uzaaji wake matunda, ulindwaji na utengemaaji wake. Kwa ajili hii amesema:

أَفَرَأَيْتُم مَّا تَحْرُثُونَ أَأَنتُمْ تَزْرَعُونَهُ أَمْ نَحْنُ الزَّارِعُونَ

“Je, mnaona mbegu mnazozipanda? Je, kwani nyinyi ndio mnaziotesha au sisi ndio Wenye kuotesha mimea?”[5]

Mpandaji wa kikweli ni Allaah. Kuhusu wewe ulichofanya ni sababu peke yake. Pengine mbegu hii ikazaa na pengine isizae. Hata ikizaa inaweza kuwa nzuri kama ambavo pengine isiwe nzuri. Kadhalika inaweza kupatwa na ugonjwa na ikakauka.

[1] 05:23

[2] 65:03

[3] 05:23

[4] 08:02

[5] 56:63-64

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 137-140
  • Imechapishwa: 28/12/2020