64. Dalili kwamba matarajio ni ´ibaadah na sharti za kukubaliwa matendo

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya matarajio ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

“Hivyo anayetaraji kukutana na Mola wake na atende matendo mema na wala asishirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote.”[1]

MAELEZO

Maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن كَانَ يَرْجُو

“Hivyo anayetaraji.. “

Bi maana anatamani juu ya thawabu za Allaah (´Azza wa Jall) na kumuona waziwazi kwa macho siku ya Qiyaamah. Yule anayetamani kumuona Allaah kwa macho siku ya Qiyaamah basi  afanye matendo mema. Afanye sababu itayomfanya kufikia mahitajio haya. Nayo ni malipo ya kuingia Peponi na kuokoka kutokamana na Moto na kutazama uso Wake mtukufu. Kwani hayo mawili ni mambo yanayokwenda sambamba. Kwa sababu yule mwenye kuingia Peponi  basi atamuona Allaah (´Azza wa Jall):

فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا

“Hivyo anayetaraji kukutana na Mola wake na atende matendo mema.”

Hii ni dalili inayoonyesha kuwa kutaraji peke yake hakutoshi. Ni lazima mtu afanye matendo. Ama kitendo cha wewe kumtarajia Allaah lakini hufanyi matendo huku ni kutumia vibaya sababu. Matarajio yenye kusifiwa ni yale yaliyoambatana na matendo. Matarajio yasiyosifiwa ni yale ambayo hayakuambatana na matendo mema. Matendo mema ni yale yaliyotimiza sharti mbili:

Ya kwanza: Kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall).

Ya pili: Kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kitendo hakiwi chema isipokuwa mpaka kitimize sharti hizi mbili. Kiwe kimefanywa kwa ajili ya Allaah peke yake na ndani yake hakina shirki. Kiwe kimepatia Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa msemo mwingine ndani yake kisiwe na Bid´ah. Kikitimiza sharti mbili hizi basi hicho ni kitendo chema. Kikikosa sharti moja basi kinakuwa kitendo kilichoharibika na kisichomfaa mwenye nacho. Kitendo ambacho ndani yake mna shirki anarudishiwa mwenye nacho. Vivyo hivyo kitendo ambacho ndani yake mna Bid´ah anarudishiwa mwenye nacho. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[2]

Aayah hii ndani yake mna matarajio na kwamba ni kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall). Faida nyingine ni kwamba matarajio peke yake hayasihi isipokuwa yakiambatana pamoja na matendo.

[1] 18:110

[2] al-Bukhaariy (7350) hali ya kuiwekea taaliki na Muslim (18) (1718).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 136-137
  • Imechapishwa: 28/12/2020