63. Dalili kwamba khofu ni ´ibaadah na mfano wa khofu ya kimaumbile

Aina ya pili ni khofu ya kimaumbile. Ni kule mtu kuogopa kitu kilicho wazi ambacho kina uwezo juu ya yale ambayo mtu anaogopa kwa ajili yake. Kwa mfano mtu akaogopa  nyoka, nge au adui. Haya ni mambo yako wazi na yenye kutambulika. Kuogopa vitu hivi sio shirki kwa sababu ni khofu ya kimaumbile kutokamana na kitu cha wazi na kinachotambulika. Kwa sababu unaogopa sababu ya wazi na kinachotakikana ni wewe kujilinda kwacho na kuchukua tahadhari kutokamana nacho kama vile kuchukua silaha na bakora kwa ajili ya kumuua nyoka, nge na wanyama wakali. Kwani hivi ni vitu vyenye kuhisiwa. Ndani yake kuna madhara yanayotambulika. Unapoviogopa vitu hivi haiitwi kuwa ni shirki. Bali inaitwa kuwa ni khofu ya kimaumbile. Kwa ajili hii Allaah amesema kuhusu Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

فَخَرَجَ مِنْهَا خَائِفًا

“Basi akatoka humo hali ya kuwa na khofu… “

Bi maana kutoka mji wake:

خَائِفًا يَتَرَقَّبُ

“… hali ya kuwa na khofu anaangaza kwa tahadhari.”[1]

Anaogopa kutokamana na maadui zake kwa sababu ameiua katika wao nafsi. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akakimbia kuelekea Madyan. Alikuwa anaanza kwa tahadhari na akiogopa wasimkamate. Hii ni khofu ya kimaumbile. Lakini kinachopasa ni mtu kushikamana na Allaah (´Azza wa Jall), achukue sababu zitazomlinda kutokamana na madhara na amtegemee Allaah (´Azza wa Jall). Amesema (Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!”[2]

Aayah hii iko katika Suurah “Aal ´Imraan” juu ya kisa cha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pamoja na washirikina siku ya Uhud pindi washirikina walipowatisha na wakasema kuwa watawarudilia na kuwakomesha. Ndipo Allaah (Jalla wa ´Alaa) akasema:

إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

”Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha marafiki zake. Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi – mkiwa ni waumini!”[3]

Bi maana vitisho hivi si vyenginevyo vinatoka kwa shaytwaan. Anawaogopesheni wapenzi wake au anawaogopesheni wale watu wenye kumnyenyekea. Hivyo anawatawala.

[1] 28:21

[2] 03:175

[3] 03:175

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 135-136
  • Imechapishwa: 28/12/2020