63. Pepo na Moto vimeshaumbwa na kamwe havitoteketea

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naamini kuwa Pepo na Moto vimeshaumbwa, hivi sasa vipo na kwamba havitomalizika.

MAELEZO

Miongoni mwa vitu vitavyokuwa siku ya Qiyaamah ni Pepo na Moto. Pepo ambayo Allaah amewaandalia wema. Moto ambao Allaah amewaandalia makafiri. Ni makazi mawili ambayo ni lazima watu waingie ndani. Ni makazi mawili ambayo yatabaki. Ni makazi yenye kuthibiti:

يَا قَوْمِ إِنَّمَا هَـٰذِهِ الْحَيَاةُ الدُّنْيَا مَتَاعٌ وَإِنَّ الْآخِرَةَ هِيَ دَارُ الْقَرَارِ

“Enyi watu wangu! Hakika maisha haya ya dunia ni starehe ya kupita tu na hakika Aakhirah ndiyo nyumba ya kutulizana milele.”[1]

Ndani yake hakuna jambo la kuhama. Wakazi wake watatulizana humo milele. Waumini watakuwa Peponi ambapo Allaah amewaandalia wachaji. Wakazi wa Motoni watakuwa ndani ya Moto ambao Allaah amewaandalia makafiri.

Kuamini Pepo na Moto inahusiana na kuamini mambo matatu ambayo ameyataja hapa:

La kwanza: Kwamba viwili hivyo vimekwishaumbwa. Amesema (Ta´ala) kuhusu viwili hivyo:

أُعِدَّتْ

“Imeandaliwa”[2]

Bi maana Nimeshaviumba na Kuviandaa. Ni viwili ambavyo vimeshaumbwa katika jumla ya uumbaji.

La pili: Vipo. Amesema (Rahimahu Allaah):

“Hivi sasa vipo.”

Ni Radd kwa wale wanaosema kuwa vitafanywa kupatikana siku ya Qiyaamah. Wanasema kuwa hivi sasa hakuna Pepo na Moto, jambo ambalo ni batili. Kwa sababu hivi vipo. Dalili ya hayo ni:

1- Allaah amesema kuhusu Pepo:

أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ

“Imeandaliwa kwa wenye kumcha Allaah.”[3]

Amesema kuhusu Moto:

أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ

“Umeandaliwa kwa makafiri.”[4]

Maneno Yake “umeandaliwa” imetajwa kwa fomu iliyokwishapita inayofahamisha kuwa umeshaumbwa. Hakusema kuwa utaumbwa au utaandaliwa. Bali amesema kuwa umeandaliwa. Ni maelezo ya kitu kilichokwishafanywa.

2- Hakika Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa yale yanayowasibu watu katika ukali wa joto au ukali wa baridi ni kutokana na Moto. Moto unapumua:

– Unapumua katika msimu wa joto. Hapa ndipo pale ambapo watu wanahisi joto kali.

–  Unapumua katika msimu wa baridi. Hapa ndipo pale ambapo watu wanahisi baridi kali.

Ni dalili inayofahamisha kuwa vipo na kwamba joto hili na baridi hii inatokana na Moto.

3- Siku moja Maswahabah walikuwa wamekaa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakasikia kitu kilichoanguka. Akasema: “Mnajua ni kitu gani?” Wakasema: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Akasema:

“Hilo ni jiwe lililotupwa ndani ya Moto tangu miaka sabini na hivi sasa ndio linaanguka ndani ya Moto mpaka lifike katika rindi lake.”[5]

 Hii ni dalili inayoonyesha kuwa Moto upo.

4- Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza kwamba maiti anapolazwa ndani ya kaburi hufunguliwa mlango wa Pepo na akajiwa na harufu yake nzuri na kwamba kafiri na mnafiki hufunguliwa mlango wa Moto na akajiwa na sumu na joto lake. Hii ni dalili inayoonyesha kuwa viwili hivyo vipo hivi sasa.

La tatu: Havitomalizika na havitoteketea kamwe. Moto utabaki na wakazi wake watabaki. Pepo itabaki na wakazi wake watabaki ndani yake bila kikomo.

Hapa kuna Radd kwa wale wanaosema kuwa Pepo na Moto vitateketea na hakuna atayebaki isipokuwa Allaah. Wanaona kuwa endapo vitabaki vitashirikiana na Allaah katika ubakiaji wake. Tunasema kuwaambia kwamba kuna tofauti kati ya kubaki kwa Muumba na kubaki kwa viumbe. Kubaki kwa Muumba ni kwa kidhati. Kuhusu kubaki kwa viumbe ni kwa ajili ya kubakizwa na Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kwa hiyo kuna tofauti kati ya viwili hivyo. Wako pia ambao wanasema kuwa Pepo itabaki lakini Moto utamalizika. Haya ni maoni pia ya makosa. Maoni ya sawa ni kwamba viwili hivyo vitabaki milele.

[1] 40:39

[2] 03:133

[3] 03:133

[4] 02:24

[5] Muslim (2844) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 91-92
  • Imechapishwa: 15/05/2021