64. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya waumini kumuona Mola wao Aakhirah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Waumini watamuona Mola wao kwa macho yao siku ya Qiyaamah kama wanavyouona mwezi usiku wenye mwezi mng´aro. Hawatosongamana katika kumtazama.

MAELEZO

Haya masuala ni miongoni mwa masuala ya siku ya Qiyaamah pia. Kwa sababu Shaykh (Rahimahu Allaah) bado ni mwenye kuendelea mambo yatayokuwa siku ya Qiyaamah. Miongoni mwa mambo hayo ni kwamba:

“Waumini watamuona Mola wao kwa macho yao siku ya Qiyaamah.”

Hii ni heshima kwao Peponi. Hakuna kitu watachohisi ni kizuri na chenye ladha zaidi kama kumtazama Allaah (´Azza wa Jall). Hiki ni kitu kimetajwa katika Qur-aan. Amesema (Ta´ala):

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya wema watapata mazuri kabisa na ziada.”[1]

Wema ni Pepo na ziada ni kutazama uso wa Allaah. Hayo yametajwa katika “as-Swahiyh” ya Muslim[2].

Vilevile amesema (Ta´ala):

لَهُم مَّا يَشَاءُونَ فِيهَا وَلَدَيْنَا مَزِيدٌ

“Watapata humo wayatakayo na Kwetu kuna yaliyo ziada.”[3]

Nyongeza ni kutazama kwao uso wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Hayo yametajwa katika tafsiri za Qur-aan[4].

Vilevile amesema (Ta´ala):

وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ

“Kuna nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Mola wake.”[5]

Nyuso zenye kung´ara zitakuwa zikimtazama Allaah kwa macho yao. an-Naadhwirah kukifuatiwa na “Ilaa” maana yake ni kutazama kwa macho. Macho ya waumini watamtazama Mola wao (´Azza wa Jall).

Vivyo hivyo maneno Yake (Ta´ala) kuhusu makafiri:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Sivyo hivyo! Hakika wao Siku hiyo bila shaka watazuiwa wasimuone Mola wao.”[6]

Bi maana hawatomuona Allaah siku ya Qiyaamah. Ni dalili inayothibitisha kuwa waumini watamuona Allaah. Kwa sababu akjizuia kutokamana na makafiri inafahamisha kuwa waumini hatojizuia nao. Hayo yamesemwa na Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah)[7]. Vinginevyo kusingelikuwa na tofauti. Lau kama Allaah asingelionekana siku ya Qiyaamah basi asingefanya kutowaona ni jambo maalum kwa makafiri. Amesema:

كَلَّا إِنَّهُمْ عَن رَّبِّهِمْ يَوْمَئِذٍ لَّمَحْجُوبُونَ

“Sivyo hivyo! Hakika wao Siku hiyo bila shaka watazuiwa wasimuone Mola wao.”

Kuhusu Hadiyth ni nyingi sana zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Amezitaja Imaam na ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake “Haadil-Arwaah ilaa Bilaad-il-Afraah”[8]. Amezitafiti Hadiyth zilizopokelewa kuhusu kuonekana kwa Allaah na kwamba zimefikisha kiwango cha kupokelewa mapokezi tele (Mutawaatir).

[1] 10:26

[2] Muslim (181) kupitia kwa Swuhayb (Radhiya Allaahu ´anh).

[3] 50:35

[4] Tafsiyr-ut-Twabariy (26/173-174) na Tafsiyr-ul-Qurtwubiy (17/21-22).

[5] 75:22-23

[6] 83:15

[7] al-Bayhaqiy katika ”al-I´tiqaad” uk. 132.

[8] Uk. 205 na yaliyo baada yake.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 93-94
  • Imechapishwa: 15/05/2021