62. Njia mbili zenye nguvu katika Aayah zinazothibitisha ukafiri wa mwenye kuacha swalah

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amesema:

“Haridhii isipokuwa Tawhiyd… ”

Hayuko radhi juu ya mshirikina. Yuko radhi kwa watu wa Tawhiyd. Maneno yake:

“… wala haidhinishi isipokuwa wapwekeshaji.”

Hatotoa idhini juu ya wenye kuombewa isipokuwa kwa wale wenye kumwabudu Allaah pekee. Maneno yake:

“Washirikina hawana fungu lolote la uombezi.”

Amesema (Ta´ala):

فِي جَنَّاتٍ يَتَسَاءَلُونَ عَنِ الْمُجْرِمِينَ مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ

“Katika mabustani wanaulizana kuhusu wahalifu [watawauliza:] “Nini kilichokuingizeni ndani ya Moto?” Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa wanaoswali.”[1]

Miongoni mwa sababu zilizowafanya watu kuingia Motoni ni kwamba hawakuwa miongoni mwa wenye kuswali. Hiyo imefahamisha kwamba yule mwenye kuacha swalah kwa kukusudia anakuwa kafiri ambaye atadumishwa Motoni milele. Hapa kuna Radd kwa wale wanaosema kwamba kuacha swalah ni ukafiri aina ndogo. Bali ni ukafiri aina kubwa kwa dalili ya Aayah hii:

قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ وَلَمْ نَكُ نُطْعِمُ الْمِسْكِينَ

“Watasema: “Hatukuwa miongoni mwa waswalii na wala hatukuwa tunalisha masikini.”[2]

 Bi maana hawakuwa wanaswali na wala hawakuwa wakitoa zakaah. Swalah na zakaah ni mambo mawili yanayokwenda sambamba ndani ya Qur-aan. Ni dalili iliyofahamisha kwamba kuacha swalah ni ukafiri kwa njia mbili:

Ya kwanza: Allaah ametaja kuacha swalah pamoja na mambo haya ambayo ni ukafiri kwa maafikiano:

– Kukufuru siku ya malipo, jambo ambalo ni kufuru kwa maafikiano.

– Kujizuia kutoa zakaah hali ya kupinga, jambo ambalo ni kufuru kwa maafikiano.

– Kuzishambulia Aayah za Allaah (´Azza wa Jall), jambo ambalo ni kufuru kwa maafikiano.

Kwa hiyo ni dalili iliyofahamisha kwamba kuacha swalah ni ukafiri kwa sababu kumeambatanishwa na mambo haya.

Ya pili: Amesema:

فَمَا تَنفَعُهُمْ شَفَاعَةُ الشَّافِعِينَ

“Basi haitowafaa uombezi wowote wa waombezi.”[3]

Ni dalili inayofahamisha kwamba mwenye kuacha swalah kwa makusudi hatokubaliwa uombezi. Kafiri ndiye hakubaliwi uombezi. Angelikuwa muumini basi uombezi juu yake ungekubaliwa.

[1] 74:40-43

[2] 74:43-44

[3] 74:48

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 90
  • Imechapishwa: 15/05/2021