63. Dalili ya kuendelea kwa Hijrah na kuenea kwa Ujumbe wa Muhammad

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili juu ya Hijrah kutoka katika Sunnah, ni kauli yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hijrah haitosimama mpaka Tawbah isimamishwe na tawbah haitosimamishwa mpaka jua lichomoze kutoka magharibi.”[1]

Wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotulia Madiynah, alifaradhishiwa Shari´ah zingine za Kiislamu. Kwa mfano zakaah, swawm, hajj, adhaana, Jihaad, kuamrisha mema na kukataza maovu na Shari´ah zingine za Kiislamu. Aliyafanya haya kwa miaka kumi. Baada ya hapo akafa, lakini dini yake imebaki.

Hii ndio dini yake. Hakuna kheri yoyote isipokuwa amewaonesha nayo Ummah wake, na hakuna shari yoyote isipokuwa amewatahadharisha nayo. Kheri [kubwa] aliyowaonesha nayo ni Tawhiyd na kila anachokipenda Allaah na kukiridhia. Na shari [kubwa] aliyowatahadharisha nayo ni shirki na kila anachokichukia Allaah na kukikataa. Allaah amemtuma kwa watu wote…

MAELEZO

Shari´ah zote hizi zilifaradhishwa Madiynah.

Ujumbe wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kwenda kwa majina na watu. Kwa hivyo mwenye kusema kuwa Ujumbe wake ni kwa watu peke yao au akasema kuwa kuna Mtume mwingine atakayekuja baada yake, basi huyo ni kafiri kwa maafikiano ya waislamu. Allaah (Ta´ala) amesema:

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.”[2]

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.”[3]

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا

“Na Hatukukutuma isipokuwa kwa watu wote hali ya kuwa ni mbashiriaji na muonyaji.”[4]

تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَى عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا

“Amebarikika Yule ambaye ameteremsha Pambanuzi kwa mja Wake ili awe ni muonyaji kwa walimwengu.”[5]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Nimetumilizwa kwa watu wote.”

Kila Mtume alikuwa akitumwa kwa watu wake maalum. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumwa kwa watu wote na vivyo hivyo ametumwa kwa majini. Hizi ni miongoni mwa sifa maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] Abu Daawuud (2479).

[2] 33:40

[3] 07:158

[4] 34:28

[5] 25:01

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 101-102
  • Imechapishwa: 16/02/2023