63. Adabu ya tatu iliyopendekezwa: ´Ibaadah za sunnah kwa wingi

Miongoni mwa adhabu za funga zilizopendekezwa ni kusoma Qur-aan, kufanya Adhkaar, kuomba du´aa, kuswali na kutoa swadaqah kwa wingi. Katika “as-Swahiyh” ya Ibn Huzaymah na Ibn Hibbaan wamepokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu aina tatu hazirudishwi nyuma du´aa zao; mfungaji mpaka afutari, kiongozi mwadilifu na du´aa ya mwenye kudhulumiwa ambapo Allaah huinyanyua juu ya mawingu na kuifungulia milango ya mbingu na Mola husema:

“Naapa kwa ushindi na utukufu Wangu nitakunusuru ijapo hapo baadaye.”

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy[1].

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza:

“Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mkarimu zaidi wa watu. Ramadhaan alikuwa mkarimu zaidi wakati anapokutana na Jibriyl ambapo anamfunza Qur-aan.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati anapokutana na Jibriy alikuwa mkarimu zaidi wa kheri kuliko upepo uliotumwa. Ukarimu wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ulikuwa ukikusanya aina zote za kheri katika kujitolea kwa elimu, nafsi na mali kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa ajili ya kuidhihirisha dini yake, kuwaongoza waja wake na kuwafikishia manufaa kwao kwa kila njia. Akimfunza mjinga, kuwatatulia haja na kumlisha mwenye njaa. Ukarimu wake ulikuwa unaongezeka katika Ramadhaan kutokana na utukufu wa wakati wake, kuongezewa ujira wake na kuwasaidia wafanya ´ibaadah katika ´ibaadah zao. Hivyo anakusanya kati ya kufunga na kulisha chakula, mawili hayo ambayo ni miongoni mwa sababu ya kuingia Peponi.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ni nani kati yenu hii leo ameamka akiwa ni mwenye kufunga?” Abu Bakr akasema: “Mimi.” Akauliza tena: “Ni nani kati yenu hii leo amesindikiza jeneza?” Abu Bakr akasema: “Mimi.” Akauliza tena: “Ni nani kati yenu hii leo amemlisha maskini?” Abu Bakr akasema: “Mimi.” Akauliza tena: “Ni nani kati yenu hii leo amemtembelea mgonjwa?” Abu Bakr akasema: “Mimi.” Nidipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hayakusanyiki kwa mtu isipokuwa huingia Peponi.”

[1] Ndani yake kuna udhaifu. Baadhi ya mambo yake yako na shawahidi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 77-79
  • Imechapishwa: 27/04/2021