04. Soksi za ngozi zinaweza kupanguswa kwa muda kiasi gani?

Swali 04: Soksi za ngozi zinaweza kupanguswa kwa muda kiasi gani?

Jibu: Jambo hili ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo watu wanahitajia kubainishiwa. Kwa hivyo nitafanya jibu kuwa refu zaidi kuliko swali.

Kupangusa juu ya soksi za ngozi ni kitu kimethibiti ndani ya Qur-aan na Sunnah. Kuhusu Qur-aan, Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُؤُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ

“Enyi mlioamini!  Mnaposimama kwa ajili ya swalah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka kwenye visugudi, na panguseni kwa [kupaka maji] vichwa vyenu na miguu yenu hadi vifundoni.”[1]

Maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَأَرْجُلَكُمْ

“… na miguu yenu…”

inaweza kusomwa kwa visomo viwili vilivyosihi kutoka kwa Mtume wa Allaah:

Cha kwanza:

وَأَرْجُلَكُمْ

“… na miguu yenu…”

Katika hali hii miguu yenu وَأَرْجُلَكُمْ ni mwongezo wa mashirikiano ya nyuso zenu وُجُوهَكُمْ, hivyo ina maana ya kwamba inatakiwa kuoshwa.

Cha pili:

وَأَرْجُلِكُمْ

“… na miguu yenu…”

Katika hali hii miguu yenu وَأَرْجُلِكُمْ ni mwongezo wa mashirikiano ya vichwa vyenu بِرُؤُوسِكُمْ, ikiwa na maana ya kwamba inatakiwa kupanguswa. Kutokana na visomo viwili miguu inaweza ima kuoshwa au kupanguswa. Sunnah imebainisha ni lini miguu inatakiwa kuoshwa na ni lini inatakiwa kupanguswa. Miguu inaoshwa pale ambapo inakuwa peku na kunafutwa juu yake pindi imefunikwa na soksi ya ngozi na mfano wake.

Ama kuhusiana na Sunnah, kitendo hicho kimepokelewa kwa mapokezi mengi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanazuoni wamelizingatia ni miongoni mwa yale mambo yaliyopokelewa kwa njia nyingi. Mshairi amesema:

Miongoni mwa Hadiyth zilizopokelewa kwa njia nyingi ni “Mwenye kusema uongo”

“Mwenye kujenga msikiti kwa ajili ya Allaah na akatarajia malipo”

Kuonekana kwa Allaah [Aakhirah], uombezi na Hodhi

Kupangusa juu ya soksi za ngozi na nyenginezo

Kwa hivyo kupangusa juu ya soksi ni miongoni mwa mambo yaliyopokelewa lukuki kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bora ni mtu kufuta juu ya soksi akiwa mtu amezivaa katika hali ya twahara kuliko kuzivua na kuosha miguu. Wakati al-Mughiyrah bin Shu´bah (Radhiya Allaahu ´anh) alipoinama kwa ajili ya kutaka kuvua soksi za ngozi za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi alipokuwa anataka kutawadha alimwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ziache. Nilizivaa nikiwa katika hali ya twahara” na hivyo akapangusa juu yake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kupangusa juu ya soksi kuna sharti kadhaa:

Ya kwanza: Azivae akiwa na twahara kamili kutokamana na hadathi ndogo na hadathi kubwa. Kama alizivaa wakati ambapo hakuwa na twahara basi haitosihi kufuta juu yake.

Ya pili: Upangusaji uwe ndani ya muda wa kupangusa, kama itavokuja ubainifu wake.

Ya tatu: Kupangusa kuwe kwa mnasaba wa hadathi ndogo, bi maana katika wudhuu´. Kama mtu analazimika kuoga josho kubwa basi analazimika kuzivua ili aoshe mwili wake mzima. Kwa ajili hii haiwezekani kupangusa juu ya soksi za ngozi wakati mtu ana josho la janaba. Swafwaan bin ´Assaal (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akituamrisha pindi tunapokuwa katika safari tusivue soksi zetu za ngozi kwa michana mitatu na nyusiku zake isipokuwa tu wakati wa janaba.”[2]

Ameipokea an-Nasaa’iy, at-Tirmidhiy na Ibn Khuzaymah.

Sharti hizi tatu ni miongoni mwa sharti za kusihi kupangusa juu ya soksi.

Kuhusu muda, ni mchana mmoja na usiku wake kwa ambaye ni mkazi na michana mitatu na nyusiku zake kwa ambaye ni msafiri. Kinachozingatiwa sio idadi ya swalah atakazoswali. Kinachozingatiwa ni wakati. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemuwekea mwenyeji muda wa mchana na usiku wake na msafiri muda wa michana mitatu na nyusiku zake. Mchana na usiku wake vina masaa ishirini na nne na michana mitatu na nyusku zake vina masaa sabini na mbili.

Lakini muda huu unaanza wakati gani? Muda huu unaanza kuanzia pale mara ya kwanza ataanza kupangusa. Muda haunzi kuhesabiwa kuanzia pale ambapo mtu anavaa soksi za ngozi au pale tu mara ya kwanza anapochengukwa na wudhuu´. Shari´ah imetaja neno “upangusaji” na ufutaji kuthibitishwa mpaka utokee kikweli. Ni lazima kupatikane jambo la kupangusa, jambo ambalo halipatikani isipokuwa katika ule upangusaji wa kwanza. Yakimalizika masaa ishirini na nne kuanzia ule upangusaji wa kwanza basi umemalizika muda wa kupangusa kwa yule ambaye ni mwenyeji na yakimalizika masaa sabini na mbili kuanzia ule upangusaji wa kwanza basi umemalizika muda wa kupangusa kwa yule ambaye ni msafiri. Hebu wacha tupiga mfano wa mambo hayo ili mambo yapate kubainika zaidi:

Mtu ametawadha kwa ajili ya Fajr. Baada ya hapo akavaa soksi za ngozi. Kisha akabaki na wudhuu´ wake mpaka akaswali Dhuhr na ´Aswr. Baada ya ´Aswr, saa 17.00, akatawadha kwa ajili ya Maghrib ambapo akafuta juu ya soksi za ngozi. Inafaa kwa mtu huyu kufuta mpaka 17.00 siku ya pili.  Endapo hiyo siku ya pili atapangusa saa 16.45 na akabaki na wudhuu´ wake mpaka akaswali Maghrib na ´Ishaa, basi kwa kipindi hicho atakuwa ameswali Dhuhr, ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa katika ile siku ya kwanza na Fajr, Dhuhr, ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa katika ile siku ya pili. Kwa hivyo ameswali swalah tisa. Kwa ajili hiyo tumepata kufahamu kuwa hakuzingatiwi idadi ya swalah anazoswali mtu, kama wanavofahamu wajinga wengi. Wanasema kuwa mtu akipangusa basi anaruhusiwa kuswali swalah tano za faradhi. Kitu hiki hakina msingi. Shari´ah imeweka muda wa mchana na usiku wake na muda huo unaanza kuhesabiwa kuanzia ule upangusaji wa kwanza.

Kutokana na mfano huo inapata kufahamika kwamba mtu akipangusa baada ya kumalizika kwa muda wa ufutaji basi upangusaji huo ni batili na wala hauondoshi hadathi. Lakini akifuta kabla ya kumlizika kwa muda wa kupangusa kisha akaendelea kuwa na twahara baada ya kumalizika muda wa kupangusa, wudhuu´ wake hauchenguki. Bali ataendelea kubaki na twahara yake mpaka uchenguke kwa kupatikana moja ya vichenguzi vya wudhuu´. Maoni yanayosema kuwa wudhuu´ unachenguka kwa kumalizika kwa muda wa kupangusa hayana dalili. Kumalizika kwa muda wa kupangusa maana yake ni kwamba haifai kufuta juu yake baada ya kumalizika muda wa kupangusa, na si kwamba twahara inachenguka. Ikiwa ambacho kimewekewa muda maalum wa kupangusa ni ule ufutaji, na si ile twahara, basi hakuna dalili inayoonyesha kuwa twahara imechenguka kwa sababu tu muda wa kupangusa umemalizika. Mtu huyu ametawadha wudhuu´ sahihi kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah. Mambo yakishakuwa hivo, basi hatuwezi kusema kuwa wudhuu´ huu umechenguka pasi na dalili sahihi ya ki-Shari´ah. Hakuna dalili inayoonyesha kuwa wudhuu´ unachenguka kwa kumalizika kwa muda wa kupangusa. Kutokana na hilo twahara yake bado ni yenye kuendelea kubaki mpaka uchenguke kwa kupatikana moja katika vichenguzi vya wudhuu´ ambavo vimethibiti kwa Qur-aan, Sunnah au maafikiano.

Kuhusu msafiri, inafaa kwake kufuta kwa michana mitatu na nyusiku zake ikiwa ni sawa na masaa sabini na mbili. Muda huu unaanza kuhesabiwa kuanzia ule upangusaji wa kwanza. Kwa ajili hiyo Hanaabilah (Rahimahumu Allaah) wanasema iwapo mtu atavaa soksi za ngozi akiwa katika mji wake, wudhuu´ wake ukamchenguka akiwa katika mji wake, halafu akasafiri na akapangusa kwa mara ya kwanza baada ya kuwa ameshaanza safari basi atakamilisha upangusaji katika hali ya usafiri. Haya yanajulisha kuwa maoni yanayosema kuwa muda wa kupangusa unaanza kuhesabiwa pale tu mara ya kwanza ambapo wudhuu´ unachenguka ni dhaifu.

Kitu kinachobatilisha kupangusa juu ya soksi za ngozi ni kumalizika kwa ule muda wa kupangusa na pia pale atakapozivua. Akivua soksi za ngozi basi kubatilika kule kuendelea kupangusa lakini twahara yake bado ni yenye kubaki. Dalili juu ya kwamba kuvua soksi za ngozi kunabatilisha kule kufuta ni Hadiyth ya Swafwaan bin ´Assaal:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akituamrisha pindi tunapokuwa katika safari tusivue soksi zetu za ngozi kwa michana mitatu na nyusiku zake isipokuwa tu wakati wa janaba.”

Ikafahamisha kwamba kule kuvua soksi za ngozi zilizopanguswa kunabatilisha ule upangusaji. Hiyo ina maana kwamba hawezi kurudi kuzivaa na akapangusa juu yake isipokuwa baada ya kutawadha kwa mara nyingine. Katika hali hiyo atatakiwa kutawadha wudhuu´ kamilifu na aoshe miguu miwili. Ama ile twahara yake akizivua bado ni yenye kuendelea kubaki. Twahara haichenguki kwa kuvua kile kilichofutwa juu yake. Kwa sababu mtu huyu ametawadha kwa mujibu wa dalili ya ki-Shari´ah. Mambo yakishakuwa hivo, basi hatuwezi kusema kuwa wudhuu´ huu umechenguka pasi na dalili sahihi ya ki-Shari´ah. Hakuna dalili inayoonyesha kuwa wudhuu´ unachenguka akivua kile kilichofutwa juu yake. Hakika si venginevo dalili inaonyesha tu kwamba akivua kile kilichopanguswa juu yake basi kunabatilika kule kuendelea kufuta. Ina maana kwamba hawezi kurudi kufuta kwa mara nyingine isipokuwa mpaka baada ya kutawadha wudhuu´ kamili ikiwa ni pamoja na kuosha miguu. Kujengea juu ya haya tunasema kuwa kimsingi ni kwamba twahara hii inayotokana na dalili ya ki-Shari´ah ni yenye kubaki mpaka kuthibiti dalili inayoonyessha kinyume chake. Muda wa kuwa hakuna dalili basi wudhuu´ wake ni wenye kubaki na haujachenguka. Haya ndio maoni yenye nguvu kwa mtazamo wetu.

[1] 05:06

[2] at-Tirmidhiy (96), an-Nasaa´iy (127) na Ibn Maajah (478).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/159-163)
  • Imechapishwa: 27/04/2021