05. Inafaa kupangusa juu ya soksi za ngozi kwa ajili ya kuswali tu vipindi vitano vya swalah?

Swali 05: Ni jambo lililoenea kwa wale watu wasiokuwa na elimu kwamba wanapangusa juu ya soksi za ngozi wakati wa vile vipindi vya swalah tano peke yake. Je, kitendo chao ni sahihi?

Jibu: Ni kweli hili ni jambo lililoenea kwa watu wasiokuwa na elimu. Wanafikiri kuwa kwa vile kupangusa kumewekewa muda wa mchana na usiku wake basi hiyo maana yake ni kwamba haifai kupangusa isipokuwa katika vile vipindi vya swalah tano peke yake. Hili si sahihi. Muda uliowekwa kwa mchana na usiku wake maana yake ni kwamba inafaa kwake kufuta mchana mzima na usiku wake ni mamoja ikiwa ataswali swalah tano au zaidi. Muda unaanza kuhesabiwa kuanzia ule upangusaji wa kwanza. Kuna uwezekano akaswali swalah kumi na zaidi ya hapo. Nitaleta mfano wa hilo:

Mtu amevaa soksi za ngozi katika swalah ya Fajr siku ya jumatatu. Akabaki na twahara yake mpaka alipoenda kulala usiku wa kuamkia jumanne. Kisha akapangusa kwa mara ya kwanza kwa ajili ya kuswali swalah ya Fajr siku ya jumanne kwa mfano saa 05.00 ya asubuhi. Hapa inafaa kwake kuendelea kupangusa kitambo kidogo kabla ya kufika saa 05.00 siku ya jumatano. Katika hali hii mtu huyu siku ya jumatatu atakuwa ameswali Fajr, Dhuhr, ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa kwa soksi zake za ngozi. Muda wote huu hauhesabiwi kwa sababu hajaanza kupangusa. Siku ya jumanne ameswali Fajr na akapangusa, Dhuhr na akapangusa, ´Aswr na akapangusa, Maghrib na akapangusa na ´Ishaa na akapangusa. Vilevile anaweza kupangusa siku ya jumatano kabla ya kumalizika muda wa kupangusa. Kwa mfano siku ya jumanne amepangusa saa 05:00 ya asubuhi na akaswali Fajr na halafu akapangusa siku ya jumatano saa 04:45 na akabaki na twahara yake mpaka aliposwali ´Ishaa usiku wa kuamkia alkhamisi. Katika hali hii atakuwa kwa wudhuu´ huu siku ya jumatano ameswali Fajr, Dhuhr, ´Aswr, Maghrib na ´Ishaa. Hii ina maana kuwa ameswali swalah kumi na tano tokea pale alipovaa soksi zake. Kwa sababu alizivaa kabla ya swalah ya Fajr siku ya jumatatu na akabaki na wudhuu´ wake na hakuanza kupangusa isipokuwa katika swalah ya Fajr siku ya jumanne saa 05:00 ya asubuhi na akabaki na wudhuu´ wake mpaka katika swalah ya Fajr siku ya jumatano saa 04:45 na akabaki na twahara yake mpaka aliposwali ´Ishaa ya siku hiyo. Atakuwa ameswali swalah kumi na tano.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/163-164)
  • Imechapishwa: 27/04/2021