06. Kuna sharti zipi za kupangusa juu ya soksi za ngozi?

Swali 06: Kuna sharti zipi za kupangusa juu ya soksi za ngozi?

Jibu: Kupangusa juu ya soksi za ngozi kumeshurutishwa sharti nne:

1 – Awe amevizaa wakati akiwa na twahara. Dalili ya hilo ni kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia al-Mughiyrah bin Shu´bah:

“Ziache. Nilizivaa nikiwa katika hali ya twahara” na hivyo akapangusa juu yake.”

2 – Soksi za ngozi ziwe ni safi. Zikiwa najisi basi haitojuzu kufuta juu yake. Dalili ya hilo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku moja aliwaswalisha Maswahabah zake ilihali amevaa viatu na akavivua na huku yuko anaswali na akaeleza kwamba Jibriyl amemjuza kuwa vilikuwa na taka au uchafu[1]. Hii inafahamisha kuwa haijuzu kuswali na kitu chenye najisi. Kitu kingine ni kwamba mtu akipangusa juu ya najisi kwa maji basi kile chenye kupanguswa kitachafuka kwa najisi na hivyo hazitosafika.

3 – Mwenye kupangusa awe na hadathi ndogo na si katika hali ya josho ya janaba au hali inayowajibisha kuoga. Dalili ya hilo ni Hadiyth ya Swafwaan bin ´Assaal (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akituamrisha pindi tunapokuwa katika safari tusivue soksi zetu za ngozi kwa michana mitatu na nyusiku zake isipokuwa tu wakati wa janaba.”[2]

Hivyo kupangusa kumeshurutishwa kuwe katika hali ya hadathi ndogo. Haijuzu kupangusa katika hali ya hadathi kubwa kama ilivokuja katika Hadiyth ambayo tumeitaja.

4 – Kupangusa kuwe ndani ya ule muda wa kupangusa uliowekwa katika Shari´ah.  Ni mchana na usiku wake kwa ambaye ni mkazi. Michana mitatu na nyusiku zake kwa ambaye ni msafiri. ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amefanya mkazi kupangusa mchana na usiku wake na msafiri michana mitatu na nyusiku zake.”[3]

Ameipokea Muslim.

Bi maana muda wa kupangusa juu ya soksi za ngozi. Hizi ndio sharti zilizowekwa kwa ajili ya kupangusa juu ya soksi za ngozi. Zipo vilevile sharti zengine zilizotajwa na wanazuoni, lakini zinahitajia kuangaliwa vizuri.

[1] Abu Daawuud (650).

[2] at-Tirmidhiy (96), an-Nasaa´iy (127) na Ibn Maajah (478).

[3] Muslim (276).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Buhuuth wa Fataawaa fiyl-Mas´h ´alaal-Khuffayn, katika Majmuu´-ul-Fataawaa (11/164-165)
  • Imechapishwa: 27/04/2021