Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Yule mwenye kukutana na Allaah baada ya kufanya dhambi inayopelekea kuadhibiwa Motoni ilihali ametubia na sio mwenye kuendelea juu yake, Allaah anamsamehe. Anakubali tawbah kutoka kwa waja Wake na anayasamehe madhambi.

MAELEZO

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah, kwa sababu wameitambua Qur-aan, wakaifahamu maana yake na kuifanyia kazi. Kadhalika wameitambua Sunnah na kuifanyia kazi. Kwa hivyo wametambua kuwa mwenye kutubia kutokana na dhambi ni kama hana dhambi yoyote. Ambaye atafanya dhambi na akatubi, Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) humkubalia tawbah yake.

Kuhusu madhambi madogo yanayofanywa na waislamu, waumini na wafanyao ihsaan, yanasamehewa kwa matendo mema. Yanafutwa kwa twahara, swalah, hajj, wudhuu´ na mfano wa matendo kama hayo. Kuhusu madhmbi madogo hayasamehewi isipokuwa kwa tawbah. Kwa hivyo yule mwenye kufanya madhambi makubwa, akitubu kwa Allaah basi Allaah humsamehe na humbadilishia maovu yake kuwa matendo mema. Akifa hali ya kuwa bado ni mwenye kuendelea katika hali hiyo, anastahiki kuadhibiwa na wakati huohuo wako chini ya matakwa ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Akitaka atawarehemu na akitaka atawaadhibu:

إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا

“Mkijiepusha madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu.”[1]

وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ وَيَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ

”Naye ndiye Ambaye anapokea tawbah kutoka kwa Waja Wake na anasamehe maovu na anayajua mnayoyatenda.”[2]

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

“Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akanyooka barabara.”[3]

Kwa hivyo Allaah anasamehe kwa kutubia juu ya dhambi kubwa. Mwenye kufa pasi na kutubia ilihali ni mpwekeshaji, yuko chini ya utashi wa Allaah. Kwa msemo mwingine akitaka kumsamehe atamsamehe na hatomwiniza Motoni, na akitaka kumuadhibu atamuadhibu kwa kiasi cha madhambi yake. Kisha baadaye kutokana na fadhilah na rehema za Allaah, na halafu kwa uombezi wa waombezi atamtoa Motoni na kumwingiza Peponi. Pepo ndio itakuwa makazi yake ya mwisho kutokana na upwekeshaji na matendo yake. Hizo ni fadhilah za Allaah anazomtunuku amtakaye. Hakika Allaah ni Mwingi wa fadhilah.

Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Allaah amewafanya kuifahamu haki na kuifanyia kazi, kuitetea na kuieneza kati ya watu kwa sababu ya kutaraji thawabu za Allaah na kuogopa adhabu Zake.

Aidha ni wajibu kutambua na kuamini kwamba mwenye kufa hali ya kuwa ni mshirikina ushirikina mkubwa, unafiki mkubwa au zandiki, ametoka katika Uislamu na hivyo atakuwa ni mafuta ya Motoni – ni makazi mabaya yaliyoje ya kuishilia!

[1] 4:31

[2] 42:25

[3] 20:82

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 141-142
  • Imechapishwa: 22/06/2026