Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Yule mwenye kukutana Naye baada ya kutekelezewa adhabu ya dhambi yake hapa duniani, basi hiyo ndio kafara yake. Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yule mwenye kukutana Naye baada ya kutekelezewa adhabu ya dhambi yake hapa duniani, basi hiyo ndio kafara yake. Hivyo ndivyo ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

MAELEZO

Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba zile adhabu zilizowekwa katika Shari´ah zinafuta madhambi, muda wa kuwa hajahalalisha dhambi yake na hajakufa katika hali hiyo bila ya tawbah. Kwa mfano mtu amekusudia kumuua muumini na akaona kuwa ni halali kumuua na akafa juu ya imani hiyo mbovu. Huyu amehalalisha kitu ambacho kinatambulika vyema katika Uislamu kuwa ni haramu. Mtu huyu akiadhibiwa kwa kuuliwa, dhambi yake haisamehewi. Mambo yalivyo ni kwamba dhambi yenye kusamehewa ni ya yule muislamu mtenda dhambi ambaye anatambua dhambi yake na hakuihalalisha. Adhabu za Kishari´ah zinafuta tu madhambi ambayo mtu haonelei kuwa ni halali ingawa mtenda dhambi hakutubia juu ya dhambi yake. ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhiwa sallam) amesema:

“Nipeni kiapo ya kwamba hamtomshirikisha Allaah na chochote, hamtoiba, hamtozini, hamtowaua watoto wenu, wala hamtoleta usingiziaji wa kashfa mlioizua baina ya mikono yenu na miguu yenu na wala kwamba hamtoniasi katika mema. Yule atakayeyahakikisha hayo basi ujira wake uko kwa Allaah. Yule atakayefanya kitu katika hayo na akaadhibiwa duniani  basi hiyo ndio kafara yake. Yule atakayepatwa na kitu katika hayo na Allaah akawa amemsitiri, basi jambo lake liko kwa Allaah; akitaka Atamuadhibu na akitaka Atamsamehe.”[1]

Aidha miongoni mwa mambo ambayo yanatakiwa kuzinduliwa ni kwamba kuna haki tatu zinazopelekea katika mauaji:

1 – Haki ya yule muuliwaji. Haki hii haiwezi haiwezi kutekelezwa isipokuwa siku ya Qiyaamah. Haki hii inabaki kwa Allaah – na Mola wako hamdhulumu yeyote.

2 – Haki ya Allaah (´Azza wa Jall). Haki nii inasamehewa kwa tawbah, kwa sababu msamaha wa Allaah ni mpana.

3 – Haki ya familia ya yule muuliwaji. Wana khiyari ya kuchagua kama wanataka kulipiza kisasi, kusamehe burebure au kusamehe pamoja na kulipwa pesa za umwagaji damu.

Adhabu nyenginezo kama vile uzinzi, wizi, unywaji pombe, kuwatuhumu machafu wanawake wenye kujiheshimu, zinafuta madhambi ya yule mtendaji.

[1] al-Bukhaariy (3892) na Muslim (1709).

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 143-144
  • Imechapishwa: 22/06/2026