Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Atakayekutana Naye hali ya kuwa ni mwenye kuendelea juu ya madhambi yake pasi na kutubia madhambi yanayopelekea kuadhibiwa, jambo lake liko kwa Allaah; akitaka kumuadhibu Atamuadhibu na akitaka kumsamehe Atamsamehe. Hata hivyo yule atakayekutana Naye akiwa ni kafiri atamuadhibu na wala hatomsamehe.

MAELEZO

Wapwekeshaji watenda madhambi wako chini ya matakwa ya Allaah, lakini mafikio yake ya mwisho ni Peponi. Allaah akitaka atawaadhibu kwa kuwaingiza Motoni na akitaka hatowaadhibu. Yeye ndiye Atakayeamua na ndiye mtambuzi zaidi wa hali za waja Wake. Mafikio ya mwisho ya muislamu mtenda madhambi ni kuingia Peponi. Allaah atawaidhinisha waombezi wawaombee, kisha baada ya kuchomwa, watatolewa Motoni. Halafu wataoga ndani ya mto nje ya Pepo hadi miili yao ikue kama vile mbegu inavyokua kwa yale yanayoletwa na mafuriko. Baada ya hapo watarejeshewa roho zao na kuingizwa Peponi na wataona kuwa hakuna waliotunukiwa pakubwa kama wao.

Kuhusu washirikina ambao walikufa juu ya shirki kubwa, unafiki wa kiimani na uzandiki – kama vile mayahudi, manaswara, waabudia makaburi, waabudia moto na wakanamungu – na wakafa katika hali hiyo, hawana uombezi wowote na wala hawatosamehewa kwa madhambi yao. Kwa sababu Pepo imeharamishwa kwa watu kama hawa. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa lakini anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanatembea kwa mujibu wa andiko hili tukufu inayothibitisha ya kwamba Allaah hatowasamehe washirikina kabisa, pasi na kujali kutofautiana kwa shirki, matendo yao ya jinai na ukafiri wao.

[1] 4:48

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 144-145
  • Imechapishwa: 22/06/2026