61. Matarajio na khofu juu ya waislamu

Hata hivyo wanataraji Allaah atamrehemu mwenye kufanya matendo mema na kumwingiza Peponi, lakini wanachelea juu yake. Kadhalika wanakhofia juu ya mtenda madhambi kutokana na madhambi yake, lakini wanataraji kuwa Allaah atawarehemu. Kwa msemo mwingine hawawadhamini watenda mema kuingia Peponi wala watenda maovu kuingia Motoni. Kwa sababu hilo sio jukumu la mwanadamu. Wao wanashuhudia yale ambayo Allaah ameshuhudia, nayo ni kwamba waumini wataingia Peponi na kwamba makafiri, wanafiki wenye unafiki wa kiitikadi na wapagani kwamba wataingia Motoni ikiwa watakufa katika hali hizo. Ushahidi huu unatokana na dalili za Qur-aan. Allaah amewaahidi wanaume wa kiume na waumini wa kike mabustani ya Peponi – na Allaah havunji ahadi Yake:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَانَتْ لَهُمْ جَنَّاتُ الْفِرْدَوْسِ نُزُلًا خَالِدِينَ فِيهَا لَا يَبْغُونَ عَنْهَا حِوَلًا

”Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema watapata mabustani ya al-Firdaws kuwa ni mahali pao pa makaribisho; wadumu humo, hawatotaka kuihama.”[1]

Allaah amewatishia makafiri adhabu yenye kuumiza:

وَالَّذِينَ كَفَرُوا لَهُمْ نَارُ جَهَنَّمَ لَا يُقْضَىٰ عَلَيْهِمْ فَيَمُوتُوا وَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُم مِّنْ عَذَابِهَا ۚ كَذَٰلِكَ نَجْزِي كُلَّ كَفُورٍ

”Wale waliokufuru watapata moto wa Jahannam; hawatahukumiwa kifo wakafa na wala hawatawepesishiwa adhabu yake. Namna hiyo Tunavyomlipa kila mwingi wa kukufuru!”[2]

Amesema (Ta´ala) amesema kuhusu wanafiki:

إِنَّ الْمُنَافِقِينَ فِي الدَّرْكِ الْأَسْفَلِ مِنَ النَّارِ وَلَن تَجِدَ لَهُمْ نَصِيرًا

”Hakika wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto na wala hutompata kwa ajili yao mwenye kunusuru.”[3]

[1] 18:107-108

[2] 35:36

[3] 4:145

  • Muhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 139-140
  • Imechapishwa: 22/06/2026