Kuna dalili nyingi juu ya kwamba wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakifunika nyuso zao. Hapa kunafuatia baadhi ya Hadiyth na mapokezi yanayotilia nguvu jambo hilo:

1 – ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

”Baada ya kuwekwa katika Shari´ah sitara Sawdah alitoka kwa ajili ya kutekeleza haja[1]. Alikuwa ni mwanamke mkubwa ambaye hafichikani kwa ambaye alikuwa anamjua. ´Umar bin al-Khattwaab akamuona na kusema: ”Ee Sawdah! Naapa kwa Allaah! Huwezi kujificha kwetu. Tazama ni namna gani unatoka.” Akageuka na kurejea. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa nyumbani kwake. Alikuwa anakula chakula cha jioni na mkononi mwake alikuwa na mfupa wa nyama. Akaingia kwake na kusema: ”Ee Mtume wa Allaah! Nimetoka kwa ajili ya baadhi ya haja zangu na ´Umar akanambia kadhaa na kadhaa.” Ndipo Allaah akamteremshia Wahy. Wahy haukumalizika na huku yuko na mfupa wa nyama mkononi mwake. Akasema: ”Hakika mmepewa ruhusa ya kutoka kwa ajili ya mahitaji yenu.”[2]

[1] Anakusudia hijaab ya wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika maneno Yake Allaah (Ta´ala):

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ ۚ ذَٰلِكُمْ أَطْهَرُ لِقُلُوبِكُمْ وَقُلُوبِهِنَّ

”Mnapowauliza haja, basi waulizeni nyuma ya pazia. Hivyo ni utwaharifu zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao.” (33:53)

Aayah hii ni miongoni mwa zile ambazo pendekezo la ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) limeafikiana na kuteremshwa kwa Aayah ya Qur-aan. al-Bukhaariy na wengineo wamepokea kupitia kwa Anas aliyesimulia kuwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Ee Mtume wa Allaah! Nyumbani kwako anaingia mwema na muovu. Ungeliwaamrisha mama wa Waumini kujisitiri.” Ndipo Allaah akateremsha Aayah ya hijaab.”

[2] al-Bukhaariy (8/430-431), Muslim (7/6-7), Ibn Sa´d (8/125-126), Ibn Jariyr (22/25), al-Bayhaqiy (7/88) na Ahmad (6/56).

Hadiyth hii inafahamisha kuwa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alimjua Sawdah kutokana na mwili wake, jambo ambalo linafahamisha kuwa alikuwa amefunika uso. Hata ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa alikuwa akitambulika kwa ukubwa wa mwili wake. Ndio maana ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) hakupenda ajulikane kwa maumbo yake, ndipo akapendekeza asitoke nje ya nyumba yake. Hata hivyo Shari´ah yenye Hekima haikuafikiana naye mara hii kutokana na ugumu wa jambo hilo. Haafidhw Ibn Hajar (Rahimahu Allaah) amesema wakati alipokuwa akifafanua Hadiyth iliyotajwa hapo juu:

”´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alichukizwa na watu wa nje kuja nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mpaka akafikia kumwambia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Wasitiri wakezo.” Akasisitiza maoni hayo mpaka kulipoteremka Aayah ya hijaab.  Baada ya hapo akataka wasionyeshe maumbo yao kabisa, ijapo wamejisitiri, na akakazia jambo hilo. Hata hivyo pendekezo hilo likakataliwa na wakapewa ruhusa ya kutoka kwa ajili ya mahitaji yao kwa ajili ya kuondosha uzito na ugumu.”

al-Qaadhwiy ´Iyaadhw amesema:

”Kuhusiana na mama wa Waumini wao wamefaradhishiwa kufunika nyuso na mikono yao.   Haijuzu kwao kuonyesha vitu hivyo, si wakati wa ushahidi au katika mazingira mengine. Wala haifai kwao kuonyesha maumbo yao, ijapo wamejifunika, isipokuwa yale yanayopelekea dharurah.”

Haafidhw Ibn Hajar amesema:

”Kisha akajengea hoja kwa Hadiyth iliopo katika ”al-Muwattwa´” ambapo imekuja kwamba wakati ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) alipokufa, wanawake walimfunika Hafswah ili yasionekane maumbo yake. Zaynab bint Jahsh alimtengenezea kuba juu ya kibanda chake ili yasionekane maumbo yake.” (Fath-ul-Baariy (8/530))

Maneno yake kwamba walifaradhishiwa jambo hilo hayana dalili. Walikuwa wakihiji baada ya kufa kwake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Isitoshe Maswahabah na wengine waliokuja baada yao walikuwa wakisimulia Hadiyth kutoka kwao katika hali ya wao kujisitiri miili yao na si maumbo yao. Na wakati ´Atwaa´ alipotaja Twawaaf ya ´Aaishah na Ibn Jurayj akamuuliza kama ilikuwa kabla au baada ya kufaradhishwa hijaab, akajibu kuwa ilikuwa baada ya kufaradhishwa hijaab.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Jilbaab-ul-Mar-ah al-Muslimah, uk. 105-106
  • Imechapishwa: 03/10/2023