Ndugu  wapendwa! Hichi ni kikao cha pili katika kubainisha fungu la pili katika adabu za funga. Nazo ni zile adabu zilizopendekezwa. Miongoni mwazo ni:

Daku. Ni kule kula sehemu ya mwishoni ya usiku. Imepata jina hilo kwa sababu hutokea kipindi cha kabla ya kuingia alfajiri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha daku pale aliposema:

“Kuleni daku. Kwani hakika katika kula daku kuna baraka.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Muslim amepokea vilevile katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kipambanuzi kati ya funga yetu na funga ya Ahl-ul-Kitaab ni kula daku.”

Amesifia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kula daku ya tende pale aliposema:

“Neema ya daku ya muumini ni daku.”

Ameipokea Abu Daawuud[1].

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Daku yote ni baraka. Msiiache ijapo ni kwa kuweka kinywani mwake maji. Kwani hakika Allaah na Malaika Wake wanawaswalia walaji daku.”

Ameipokea Ahmad. al-Mundhiriy amesema:

“Cheni ya wapokezi wake ni yenye nguvu.”[2]

Mlaji daku anatakiwa kunuia kwa daku lake kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumwigiliza kitendo chake ili daku hiyo iwe ni ´ibaadah na anuie kwa funga yake kumcha Allaah ili apate ujira.

[1] Cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Ina shawahidi inayoifikisha katika daraja ya usahihi.

[2] Sentesi ya mwanzo ina shahidi kwa al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 75-76
  • Imechapishwa: 24/04/2021