Hedhi ina hukumu nyingi zaidi ya ishirini. Tutataja katika hizo zile zilizo na haja zaidi:

1- Swalah. Ni haramu na si sahihi kwa mwanamke mwenye hedhi kuswali swalah ya faradhi na ya sunnah. Swalah sio wajibu kwake isipokuwa ikiwa kama atadiriki katika wakati wake kiasi cha Rakaa moja. Hapo itakuwa ni wajibu kwake kuswali sawa ikiwa amediriki hilo mwanzoni mwa wakati au mwisho wake.

Mfano wa mazingira ya kwanza mwanamke amepatwa na hedhi kiwango sawa na wakati wa Rakaa moja baada ya kuzama kwa jua. Pale atapotwaharika ni wajibu kwake kuswali Maghrib kwa sababu alitwaharika kiwango cha wakati wa Rakaa moja baada ya jua kuzama.

Mfano wa mazingira ya pili mwanamke ametwaharika kiwango sawa na wakati wa Rakaa moja kabla ya kuchomoza jua. Pale atapotwaharika ni wajibu kwake kuswali Fajr kwa sababu alitwaharika kiwango cha wakati wa Rakaa moja kabla ya jua kuchomoza.

Ama mwanamke akipata hedhi na kutwaharika sehemu ya kilicho chini ya kiwango kisichomtosheleza kuswali Rakaa moja kabla ya kuzama kwa jua na kuchomoza kwa jua, swalah itakuwa sio wajibu kwake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuwahi Rakaa moja basi ameiwahi swalah.”[1]

Ina maana ya kwamba yule ambaye hatowahi Rakaa moja ya swalah basi hakuiwahi swalah.

Mwanamke mwenye kutwaharika kiwango sawa na wakati wa Rakaa moja kabla ya kutoka kwa ´Aswr na ´Ishaa ni wajibu kwake kuswali Dhuhr na ´Aswr, na Maghrib na ´Ishaa? Wanachuoni wametofautiana katika hili. Maoni sahihi ni kuwa sio wajibu kwake kuswali isipokuwa tu ile swalah aliyodiriki wakati wake, kwa hivyo ataswali ´Aswr na ´Ishaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kuwahi Rakaa moja ya ´Aswr kabla ya jua kuzama basi ameiwahi ´Aswr.”[2]

Hakusema kuwa amewahi Dhuhr na ´Aswr au kuwa ni wajibu kuswali pia Dhuhr. Asli ni kutakasika dhimma. Haya ndio maoni ya Abu Haniyfah na Maalik, kama ilivyosimuliwa katika kitabu “Sharh-ul-Muhadhdhab”[3]

Inapokuja katika Dhikr, Takbiyr, Tasbiyh, Tahmiyd, jina la Allaah wakati wa kula na mengineyo, kusoma Hadiyth na Fiqh, kuomba du´aa na kuitikia “Aamiyn” na kusikiliza Qur-aan, hakuna kilicho haramu kwake katika hayo. Imethibiti katika al-Bukhaariy, Muslim na kwengineko kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilala na kusoma Qur-aan huku ameegemea mapaja ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ilihali yuko na hedhi[4].

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kuwa Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituamrisha katika ´Iyd mbili kuwatoa wanawake chipukizi ambao ndio wametoka katika kukomaa, wanawake wenye hedhi na ambao hawajaolewa. Kuhusiana na wanawake wenye hedhi, waepuke sehemu za kuswalia.”[5]

Ama kuhusu kisomo cha Qur-aan cha ukimya bila ya kutikisa ulimi, ni sawa. Mfano wa hilo ni yeye kusoma ndani ya Msahafu au ubao bila ya kutikisa ulimi. an-Nawawiy amesema katika “Sharh-ul-Muhadhdhab:

“Hilo linajuzu pasi na tofauti yoyote. Ama ikiwa atasoma kwa kutikisa ulimi, wanachuoni wengi wanaona kuwa ni haramu.”[6]

al-Bukhaariy, Ibn Jariyr at-Twabariy na Ibn-ul-Mundhir wamesema:

“Inajuzu.”

Ibn Hajar amemnasibishia kauli hiyo Maalik na ash-Shaafi´iy katika kauli yake ya zamani[7]. al-Bukhaariy amepokea kwa mlolongo wa wapokezi uliokatika mwanzoni kwamba Ibraahiym an-Nakha´iy amesema:

“Ni sawa akasoma Aayah.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Hakuna asli katika Sunnah chenye kumzuia kusoma Qur-aan.” Hadiyth:

“Mwanamke mwenye hedhi na mwenye janaba hasomi kitu chochote katika Qur-aan.”

ni dhaifu kwa maafikiano ya wanachuoni wote wa Hadiyth[8]. Hata wanawake waliokuwa katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakipatwa na hedhi. Lau ingelikuwa kisomo cha Qur-aan ni haramu kwao kama ilivo swalah, basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliwabainishia hilo Ummah wake na kuwafundisha mama wa waumini na hivyo lingeenea kwa watu. Ilipokuwa hakuna yeyote aliyenukuu hilo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi haifai vilevile kusema kuwa ni haramu. Kwa vile hakukataza hilo. Kwa vile (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakulikataza pamoja na kuwepo kwa wanawake wengi wenye hedhi katika zama zake, mtu anapata kujua kuwa sio haramu.”[9]

Baada ya kujua maoni mbali mbali ya wanachuoni lililo salama zaidi kwa mwanamke mwenye hedhi ni kutokusoma Qur-aan kwa ulimi ikiwa hana haja ya kufanya hivo kama kufundisha au mtihani.

[1] al-Bukhaariy (580) na Muslim (607).

[2] al-Bukhaariy (579) na Muslim (608).

[3] Sharh-ul-Muhadhdhab (3/70).

[4] al-Bukhaariy (297) na Muslim (301).

[5] al-Bukhaariy (324) na Muslim (890).

[6] Sharh-ul-Muhadhdhab (2/372).

[7] Fath-ul-Baariy (1/408).

[8] at-Tirmidhiy (131).

[9] Majmuu´-ul-Fataawaa (26/191).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016