2- Swawm. Ni haramu na si sahihi kwa mwanamke mwenye hedhi kufunga swawm ya faradhi na ya sunnah. Hata hivyo ni wajibu kwake kulipa zile siku zilizompita za swawm ya faradhi. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Tulipokuwa tunapata hedhi tulikuwa tunaamrishwa kulipa swawm na wala hatuamrishwi kulipa swalah.”[1]

Akipata hedhi hali ya kuwa amefunga inabatilika hata kama itajitokeza mara tu kabla ya jua kuzama. Swawm hiyo ikiwa ni ya faradhi basi ni wajibu kwake kulipa siku hiyo.

Akiwa ni mwenye kuhisi kuwa hedhi iko njiani inakuja lakini haikutoka isipokuwa baada ya jua kuzama, swawm yake ni kamilifu. Kutokana na kauli sahihi swawm yake si yenye kubatilika. Kwa sababu damu ilioko ndani ya mwili haina hukumu yoyote. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoulizwa kama ni wajibu kwa mwanamke kuoga pale anapoota ndoto ya mapenzi akajibu kwa kusema:

“Ndio, akiona maji.”[2]

Akaambatanisha hukumu kwa kuona manii na si kwa zile hisia zake. Hali kadhalika hukumu ya hedhi inaanza kuthibiti pale damu inapoonekana.

Na akipata hedhi baada ya kuingia kwa alfajiri, swawm ya siku hiyo sio sahihi hata kama atatwaharika mara tu baada ya alfajiri.

Na akitwaharika mara tu kabla ya alfajiri basi swawm yake ni sahihi hata kama hakuoga isipokuwa baada ya alfajiri. Vivyo hivyo mwenye janaba swawm yake ni sahihi ikiwa atanuia kufunga na asioge isipokuwa baada ya alfajiri. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mwenye kuamka hali ya kuwa na janaba ya jimaa na anafunga katika Ramadhaan.”[3]

[1] al-Bukaariy (321) na Muslim (335).

[2] al-Bukhaariy (130) na Muslim (311).

[3] al-Bukhaariy (1925) na Muslim (1109).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016