Mambo yenye kuzuka wakati wa hedhi yako aina mbali mbali ikiwa ni pamoja na:

1- Inaweza kuzidi au kupungua. Kwa mfano mwanamke amezowea kupata ada yake siku sita na ikaendelea mpaka siku ya saba ambapo kuna mwingine amezowea kupata ada yake siku saba na akatwaharika kwa siku sita.

2- Inaweza kutangulia au kuchelewa. Kwa mfano ada ya mwanamke inaweza kuwa inakuja mwishoni mwa mwezi na mara akaiona mwanzoni mwa mwezi ambapo kuna mwingine amezowea kupata ada yake mwanzoni mwa mwezi na mara akaiona mwishoni mwa mwezi.

Wanachuoni wametofautiana kuhusu matokeo haya mawili. Kauli sahihi ni kwamba pale atapoona damu, basi ahesabu hiyo kuwa ni hedhi, na pindi inapokatika, ahesabu kuwa yuko twahara. Haijalishi kitu sawa ikiwa ada yake imezidi au imepungua, imetangulia au imechelewa. Dalili ya hilo imeshatangulia pale ambapo Allaah amefungamanisha hukumu za hedhi kwa kule kupatikana kwake. Haya ndio maoni ya ash-Shaafi´iy yaliyochaguliwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Ibn Qudaamah amesema kuwa maoni haya ndio yenye nguvu na akaitetea pindi aliposema:

“Lau ada ingelikuwa ni yenye kuzingatiwa kwa namna ilivyotajwa katika madhehebu basi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) angeliwabainishia Ummah wake na kutochelewesha ubainifu kwa sababu haijuzu kuchelewesha ubainifu pale inapohitajika kufanya hivo. Wakeze na wanawake wengine walikuwa ni wenye kuhitajia ubainifu wa hilo katika nyakati zote. Katu asingeghafilika kwalo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutaja si ada wala ubainifu isipokuwa damu ya ugonjwa ya mwanamke.”[1]

3- Manjano-njano au uchafu. Hali hii mwanamke anaona damu ya manjano inayofanana na maji ya majeraha au damu chafu ambayo ni mchanganyiko wa umanjano na weusi. Damu kama hii ikiwa ni ndani ya kipindi cha hedhi au ni yenye kuambatana nayo kabla ya kutwaharika, inahesabika kuwa ni hedhi na zitamthibitikia hukumu za hedhi. Hata hivyo itakuwa si hedhi ikiwa vimaji-maji hivyo vitamtoka baada ya kutwaharika. Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Tulikuwa hatuzingatii umanjano na uchafu baada ya kutwaharika kuwa ni kitu.”[2]

Ameipokea Abu Daawuud kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh. al-Bukhaariy pia ameipokea bila ya nyongeza:

“… baada ya kutwaharika…”[3]

Hata hivyo kichwa cha khabari yake ni:

“Umanjano na uchafu mbali na masiku ya hedhi.”

Ibn Hajar amesema katika ufafanuzi wake “Fath-ul-Baariy”:

“Hivyo anaashiria kuoanisha kati ya Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliyotangulia “Usifanye haraka mpaka utapoona weupe” na Hadiyth ya Umm ´Atwiyyah (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliyotajwa katika mlango huu kwa njia hiyo Hadiyth ya ´Aaishah ni yenye kutumika pale atakapoona umanjano na uchafu katika masiku ya hedhi na Hadiyth ya Umm ´Atwiyyah inatumika nje na masiku ya hedhi.”

Hadiyth ya ´Aaishah iliyoashiriwa ameipokea al-Bukhaariy kwa mkato, kwa maazimio, mlolongo wa wapokezi kabla ya mlango huu. Wanawake walikuwa wakimtumia kitu cha pamba kilicho na umanjano ambapo anasema:

“Usifanye haraka mpaka utapoona weupe.”[4]

Weupe ni maji meupe yenye kutoka ukeni wakati hedhi inapokatika.

4- Kukatika-katika katika hedhi. Ina maana ya kwamba akapata hedhi kwa siku moja tofauti na siku nyingine na mfano wa hayo. Matokeo haya yana hali mbili:

1- Mwanamke akawa anatokezewa na hili siku zote. Hapa damu hii itakuwa ni damu ya ugonjwa na ana hukumu ya mwenye damu ya ugonjwa.

2- Mwanamke akawa hatokezewi na hili siku zote; linamjia wakati fulani na wakati wa twahara yake yuko sahihi. Wanachuoni wametofautiana juu ya kipindi hiki ambapo damu inakatika. Je, ni twahara au inahesabika kuwa ni hedhi? Kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi ya madhehebu ya ash-Shaafi´iy ni kwamba inahesabika kuwa ni hedhi. Kauli hii imechaguliwa na Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah, mwandishi wa “al-Faa´iq”[5] na madhehebu ya Abu Haniyfah. Kwa sababu yale maji meupe hayaonekani katika kipindi hicho. Na lau kama mtu angelisema kuwa kipindi hicho kinahesabika kuwa ni kipindi cha twahara basi ingelikuwa na maana ile ya kabla yake na ya baada yake zote mbili ni hedhi, jambo ambalo hakuna mwenye kulisema. Kadhalika ingelikuwa na maana kuwa eda ni yenye kwisha baada ya siku tano. Vilevile kungelikuwa na shida kwa kuoga na kufanya mambo mengine katika kila siku baada ya nyingine. Shida hii haipo katika Shari´ah hii na himdi zote zinamstahiki Allaah.

Kauli inayojulikana kwa Hanaabilah ni kwamba ile damu inazingatiwa kuwa ni hedhi na kule kukatika kwa damu kunahesabika kuwa ni twahara. Isipokuwa tu ikiwa yote mawili kwa pamoja yatazidi masiku ya hedhi; katika hali hiyo ile damu iliyovuka muda itakuwa ni hedhi. Ibn Qudaamah amesema katika “al-Mughniy”:

“Maoni yanayosema kuwa ile damu inayokatika chini ya siku moja haihesabiki kuwa ni twahara yamejengwa juu ya mapokezi tuliyoyataja katika mnasaba wa nifasi. Asizingatie kipindi kilicho kifupi chini ya siku moja. Haya ndio maoni sahihi – Allaah akitaka. Kwa sababu damu ni yenye kuja na kwenda. Kuwajibisha kuoga kwa yule anayetwaharika saa baada ya saa kuna uzito usiokubalika kwa kuwa Allaah (Ta´ala) amesema:

هُوَ اجْتَبَاكُمْ وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ

“Yeye Ndiye Amekuteueni [kuwa Ummah bora kabisa] na Hakukufanyieni ugumu wowote [ule] katika Dini.” (22:78)

Ibn Qudaamah amesema:

“Kutokana na hili twahara ni yenye kuanza kuzingatiwa pale damu inapokatika kuanzia siku moja maadamu hajaona kile chenye kujulisha kwa mfano damu hiyo ni yenye kukatika mwishoni mwa ada yake au akapata maji meupe.”

Kwa hivyo maoni ya Ibn Qudaamah yako kati ya kauli hizo mbili na Allaah ndiye anajua zaidi usawa.

5- Kukauka wakati wa hedhi kwa njia ya kwamba akaona majimaji tu. Akiona jambo hili katikati ya kipindi cha hedhi au imeambatana na hedhi kabla ya kutwaharika, basi ni hedhi. Mwisho wa hali yake itapata hukumu moja kama umanjano na uchafu.

[1] al-Mughniy (1/353).

[2] Abu Daawuud (307).

[3] al-Bukhaariy (326).

[4] al-Bukhaariy (19).

[5] Hivyo ndivo alivyosema mwandishi wa “al-Inswaaf”.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’ http://www.ibnothaimeen.com/all/books/article
  • Imechapishwa: 30/10/2016