Swali: Kuna wanafunzi wanaoenda na wale walioathirika na mifumo ya Hizbiyyah, kama al-Ikhwaan al-Muslimuun na Jamaa´at-ut-Tabliygh, wanakaa nao na wanahudhuria mikusanyiko na harakati zao. Wanafanya hivo kwa miaka mingi. Hali ni ile ile hakujabadilika kitu. Je, ni sahihi? Ni upi mfumo wa Salaf katika suala hili ambalo haliko wazi kwa wengi wanaojinasibisha na mfumo wa Salaf hii leo?

Jibu: Mimi nasikitika kuona jambo jili haliko wazi kwa watu wanaoishi katika nchi hii na vitabu vya Salaf vipo mbele yao. Msimamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwa Ahl-ul-Bid´ah uko wazi kama jua. Nastaajabu kuona mambo haya hayako wazi kwao na khaswa kwa wale wanaojinasibisha na mfumo wa Salaf.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitahadharisha kukaa na Ahl-ul-Bid´ah na watu wa shari kwa jumla. Salaf walifanya hali kadhalika. Wale wanaoenda kinyume na matahadharisho haya wanajiweka katika upotevu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitahadharisha kutangamana na watu wa shari na kusema:

“Mfano wa kukaa na wema na kukaa na waovu ni kama muuza manukato na muhunzi. Muuza manukato ima akakupa au ukapata kutoka kwake harufu nzuri. Muhunzi ima akaunguza nguo zako au ukapata kutoka kwake harufu mbaya.” Ahmad (04/404), al-Bukhaariy (2101) na Muslim (2628).

Au alisema maneno kama hayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ni kwa nini hawachukui nasaha za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Kama hawaathiriki 100% basi wataathirika 90%. Hatosalimika nao na khaswa yule mkweli mwenye kusadikishwa ametahadharisha nao na akatoa mfano huu mkubwa:

وَتِلْكَ الْأَمْثَالُ نَضْرِبُهَا لِلنَّاسِ ۖ وَمَا يَعْقِلُهَا إِلَّا الْعَالِمُونَ

”Na hiyo ni mifano tunawapigia watu lakini hakuna wanaoielewa isipokuwa wenye elimu.” (29:43)

Mwanachuoni ananufaika kwa mifano inayotolewa na Qur-aan au na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yote ni Wahy.

Ni kwa nini hawachukui nasaha za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Maimamu wa Uislamu, akiwemo al-Baghawiy na as-Swaabuuniy, wametangaza maafikiano juu ya kwamba Ahl-ul-Bid´ah waliopindukia wanatakiwa kukatwa, kutwezwa na kuchukiwa. Yule anayechanganyika nao, kutangamana nao na kusimama upande wao ataathirika na njia na fikira zao na kupewa mtihani kwa kuwapaka mafuta mpaka moyo wake ufe. Mara nyingi mtu kama huyu hupinda na kujiunga nao. Hayo yamewatokea wengi tunaowajua. Hata na wao walikuwa wakijinasibisha na mfumo huu. Inasikitisha sana.

Nadharia inayosema kaa na Ahl-ul-Bid´ah na uchukue haki kutoka kwao na uache batili ni ya khatari sana. Inapelekea katika matokeo mabaya sana na mengi. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba kusoma vitabu vya Ahl-ul-Bid´ah na kukaa nao kunadhuru. Muislamu anayeiheshimu ´Aqiydah na mfumo huu ni lazima kwake kuichunga dini yake ili aihifadhi ´Aqiydah na mfumo wake. Yule mwenye kupuuza huyu jambo lake liko kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Atakuja kupata matokeo mabaya kwa kutopokea nasaha za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na maelekezo ya Salaf. Ninaapa kwa Allaah wao walikuwa na hekima, wajuzi, wenye busara zaidi na wenye kuona mbali juu ya yanayopelekea matangamano haya mabaya aliyotahadharisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 13-15
  • Imechapishwa: 30/10/2016