59. Ni misafara ipi ya kijeshi ilifanyika mwaka wa 7?

Swali 59: Ni misafara ipi ya kijeshi ilifanyika mwaka huo?

Jibu: Abu Bakr as-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ´anh) alituma msafara wa kijeshi dhidi ya Fizaarah, ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) alituma msafara wa kijeshi dhidi ya Hawaazin na msafara wa kijeshi wa Ibn Rawaahah (Radhiya Allaahu ´anh) dhidi ya Yusayr bin Razaam na waliokuwa pamoja naye waliouwawa.

Katika mwaka huohuo Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ´anh) alitumwa kwenda Juhaynah ambapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamkaripia mtu ambaye ametamka shahaadah.

Abu Hadrad (Radhiya Allaahu ´anh) alitumwa kwenda Ghaabah.

Mwaka huohuo kuliongozwa pia msafara wa kijeshi na mtu ambaye aliwaamrisha wenzake kuingia motoni ili kuwajaribu utii wao. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema kuhusiana na tukio hilo:

”Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba.”[1]

Kuna msafara mwingine wa kijeshi mwaka huo uliotumwa dhidi ya Banuu Sulaym.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akalipa ´Umrah aliyokuwa aifanye mwaka jana katika Dhul-Qa’dah. Alipokuwa njiani anareja akaishi kijumba na Maymuunah. Hakuna kitu kilichokuwepo katika Ihraam wakati wa ndoa.

Katika mwaka huohuo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimrejesha msichana wake Zaynab kwa Abul-´Aasw bin ar-Rabiy´ ambaye sasa alikuwa amesilimu. Kwa mujibu wa maoni sahihi alimrudisha kwake kutokana na ile ndoa ya kwanza.

[1] al-Bukhaariy (7258) na Muslim (1840).

  • Mhusika: ´Allaamah Haafidhw bin Ahmad al-Hakamiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Amaaliy fiys-Siyrah an-Nabawiyyah, uk. 122-124
  • Imechapishwa: 25/10/2023