Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Aliishi kwa umri wa miaka sitini na tatu, arubaini kabla ya utume na ishirini na tatu kama Nabii na Mtume. Alipewa unabii kwa [kupewa Suurah] “Iqra´” Alipewa utume kwa “al-Muddaththir”.

MAELEZO

Alipewa utume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) baada ya kukamilisha miaka arobaini. Huo ndio wakati ambao mtu anakuwa mkomavu zaidi kiakili na kimwili. Alikuwa Nabii akiwa na urmi wa miaka arobaini. Kwa hivyo kipindi cha utume na unabii kwa pamoja ilikuwa miaka ishirini na tatu. Kwa mujibu wa maoni sahihi alifariki akiwa na umri wa miaka sitini na tatu. Maoni mengine yanasema alikuwa na miaka sitini. Yako maoni mengine yanasema alikuwa na sitini na tano. Hapo ndipo Allaah akamteremshia:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ

“Soma! Kwa jina la Mola wako aliyeumba – amemuumba mtu kutokana na pande la damu linaloning’inia!”[1]

Kisha baada ya muda fulani akapewa utume kwa al-Muddaththir. Alimjia Jibriyl (´alayhis-Salaam) katika pango la Hiraa´ na huku akiabudu kwa yale aliyorithi kutoka katika dini ya Ibraahiym. Alikuwa akichukua chakula na kinywaji cha kutosha kwa nyusiku mbili au tatu. Kisha anaenda kufanya ´ibaadah katika pango. Jibriyl (´aalyhis-Salaam) alikuwa akimjia katika umbo lake akiwa na mbawa mia sita zinazofunika yote yaliyo baina ya mbingu na ardhi. Alishikwa na khofu kubwa na akamwambia:

اقْرَأْ

“Soma!”

Akamjibu:

“Sijui si mwenye kusoma” akambana.”

mpaka akamfikisha kiwango cha mwisho cha juhudi. Akamwambia asome kwa mara ya pili na akambana kwa mara ya pili mpaka akamfikisha kiwango cha mwisho cha juhudi. Mara zote hizo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikariri kuwa si mwenye kusoma. Haikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakataa kwa ajili ya kukataa tu, lakini ni kwa sababu hakuwa msomaji na wala hakujifunza kusoma. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) si msomi; hajui kusoma wala kuandika.  Wanazuoni wamesema kuwa hayo yalikuwa ni maandalizi ya kubeba Ujumbe. Kwa sababu Ujumbe ni mzigo mzito. Kisha mara ya tatu akamwambia:

اقْرَأْ بِاسْمِ رَبِّكَ الَّذِي خَلَقَ خَلَقَ الْإِنسَانَ مِنْ عَلَقٍ اقْرَأْ وَرَبُّكَ الْأَكْرَمُ الَّذِي عَلَّمَ بِالْقَلَمِ عَلَّمَ الْإِنسَانَ مَا لَمْ يَعْلَمْ

“Soma! Kwa jina la Mola wako aliyeumba – amemuumba mtu kutokana na pande la damu linaloning’inia! Soma! Na Mola wako ni Mkarimu kabisa, ambaye aliyefunza kwa kalamu, amemfunza mtu yale asiyoyajua!”[2]

Akarejea moyo wake ukitetemeka kwa kumuona Malaika hali ya kuwa na woga. Akaja kwa mke wake Khadiyjah ambaye alimwambia:

“Hapana, naapa kwa Allaah kwamba hakutotweza. Kwani hakika wewe unaunga kizazi, unamkirimu mgeni, unawasaidia wenye kukosa, unabeba mazito [ya watu] na unasaidia katika shida mbalimbali.”

Hizi ni sifa zenye kusifiwa na mwenye kusifika nazo basi Allaah kamwe hamdhalilishi. Akampa bishara na akampeleka kwa binamu yake Waraqah bin Nawfal. Alikuwa ni mtu aliyeingia katika unaswara na alikuwa akisoma katika vitabu vya kiebrania. Akamuuliza ni kipi kinachomjilia? Akasema: “Ni kadhaa na kadhaa.” Alikuwa ni mzee na ameshakuwa kipofu. Akasema: “Hii ni Namuus ambayo ilikuwa ikimjilia Muusa. Wewe ndiye Nabii wa ummah huu. Laiti ningelikuwa na kijana mwenye nguvu pindi watapokufukuza watu wako.” Kwa sababu alikuwa ameshakuwa mtumzima. Akasema: “Je, hivi kweli watanitoa?” Akasema: “Ndio. Hakuna yeyote aliyekuja na mfano wa ulichokuja nacho isipokuwa aliudhiwa.” Baada ya siku chache Waraqah  akaaga dunia.”[3]

Imepokelewa katika baadhi ya Hadiyth ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimbashiria Pepo kwa sababu alikuwa ndiye mtu wa kwanza aliyemwamini.

Kisha baada ya muda akasema:

“Nigubikeni, nigubikeni, nigubikeni, nigubikeni.”

Hapo ilikuwa baada ya kujiwa na Malaika akamwambia:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye! Na Mola wako mtukuze!”

Ndipo alikuwa Mtume. Akawaonya watu.

Kwa mujibu wa Qur-aan Tukufu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amepitia hatua mbili katika unabii na utume. Hatua mbili hizo ni zifuatazo:

1 – Unabii. Hapo ni pale kulipoteremshwaa:

اقْرَأْ

“Soma!”

Kwayo ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa Nabii.

2 – Utume. Hapo ni pale kulipoteremshwaa:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ قُمْ فَأَنذِرْ

”Ee uliyejigubika! Simama na uonye!”

Akawatahadharisha watu. Kwa kuteremshwa kwake ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa Mtume.

[1] 96:01-02

[2] 96:01-05

[3] al-Bukhaariy (03) na Muslim (160).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 91-93
  • Imechapishwa: 14/02/2023