Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

3 – Msingi wa tatu:

Ni kumtambua Mtume wenu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alikuwa ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim. Haashim alikuwa anatokamana na [kabila la] Quraysh, Quraysh ni kutokamana na waarabu na waarabu ni kutokamana na kizazi cha Ismaa´iyl, mtoto wa Ibraahiym al-Khaliyl – baraka za juu na salamu ziwe juu yake na kwa Mtume wetu.

MAELEZO

Huu ni msingi wa tatu miongoni mwa ile misingi mitatu ambayo ni lazima kwa kila muislamu kuijua, kuifanyia kazi, kulingania kwayo na kusubiri juu ya yale yatakayompata. Aidha mtu ataulizwa ndani ya kaburi lake kuhusu utambuzi wa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ana majina mengi. Miongoni mwayo, kama ilivyopokelewa kutoka kwake, ya kwamba amesema:

“Mimi ni Muhammad, mimi ni Ahmad, mimi ni mfutaji (الْمَاحِي) ambaye kwake unafutwa ukafiri, mimi ni mkusanyaji (الْحَاشِرُ) ambaye watu watakusanywa baada yangu, mimi ni wa mwisho (الْعَاقِبُ) ambaye hakuna Mtume mwingine baada yangu.”[1]

Maneno yake mtunzi (Rahimahu Allaah):

“Alikuwa ni Muhammad bin ´Abdillaah bin ´Abdil-Muttwalib bin Haashim… “

Huu ndio nasaba yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mwanahistoria Ibn-us-Swaabuuniuy[2] ameandika kuhusu nasaba yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ametaja mpaka kwa Ma´d kwa ´Adnaan, mababu hawa kuna maafikiano juu yao. Wako mababu ambao kuna tofauti juu yao ambao ni watano au wasita. Mababu hao ni baina ya ´Adnaan na Ismaa´iyl pamoja na kukubaliana ya kwamba wanatokana na kizazi cha Ismaa´iyl bin Ibraahiym kipenzi mwandani wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo nasaba yake ni yenye kujulikana. Quraysh pia ni kabila mashuhuri. Ni Mtume Haashimiy, Muttwalibiy na Haashim anatokana na Quraysh. Quraysh ni miongoni mwa makabila matukufu zaidi; anatokana na kizazi cha Ismaa´iyl (´alayhis-Salaam). Kwa sababu Ismaa´iyl ni baba wa pili na baba wa kwanza ni Ibraahiym (´alayhis-Salaam), kabla yao ni Nuuh, kabla yao ni Aadam (´alayhis-Salaam) na Aadam ndiye baba wa watu, kisha Nuuh baba wa pili ambaye aliwabeba kwenye jahazi walioamini ambao walikuwa idadi kidogo kisha wakateremka. Walipoteremka wakapotea na wakabaki watoto wa Nuuh. Amesema (Ta´ala):

وَجَعَلْنَا ذُرِّيَّتَهُ هُمُ الْبَاقِينَ

“Tukafanya dhuria wake wao ndio wenye kubakia.”[3]

Saam, Yaafith na Haam. Kisha baada ya hapo akaja Ibraahiym. Kila Kitabu ambacho Allaah alikiteremsha baada ya Ibraahiym ni cha Nabii miongoni mwa kizazi chake. Kwa hivyo Allaah akamruzuku Ibraahiym watoto wa kiume wawili; wa kwanza ni Ismaa´iyl ambaye mama yake ni Haajar ambaye mfalme wa Misri katika kipindi hicho alimzawadia Saarah. Akamzaa Ismaa´iyl akamtumainia Ibraahiym. Saarah ndiye ambaye alimpa Haajar awe mke wake. Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni katika kizazi cha Ismaa´iyl. Mkewe Saarah alikuwa ni tasa. Baadaye Allaah akamruzuku Ishaaq ambapo inasemekana ni baada ya miaka kumi na mbili. Ya´quub, ambaye ndiye israaiyl, alikuwa ni katika ukoo wa Ishaaq. Mitume wote wa wana wa israaiyl ni katika ukoo wa Ya´quub bin Ishaaq bin Ibraahiym ambapo wa mwisho wao ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu Ismaa´iyl ni katika ukoo wa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (3532) na Muslim (2354).

[2] Muhammad bin ´Aliy bin Mahmuud; Abu Haamid, Jamaal-ud-Diyn al-Mahmuudiy. Ibn-u-Swaabuuniy ni miongoni mwa wanazuoni wa Hadiyth ambaye anawatambua wapokezi wa Hadiyth. Ni mwalimu na Imaam adh-Dhahabiy. Ni miongoni mwa watu wa Dameski. Ana kitabu kaandika ”Takmilatu Ikmaal-il-Ikmaal fiy-Ansaab”. Alifariki 680 H.

[3] 37:77

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 89-90
  • Imechapishwa: 14/02/2023