Zipo alama nyingi za Qiyaamah. Miongoni mwazo ni zifuatazo:

1 – Kuipoteza swalah[1].

2 – Kuwaasi wazazi wawili[2].

3 – Kuenea kwa ala za muziki na pumbao[3].

na nyenginezo ambazo hazihesabiki. Hizi ni baadhi ya alama ndogo za Qiyaamah.

Zipo alama kubwa za Qiyaamah zinazofuatia alama ndogo:

1 – Kujitokeza kwa al-Mahdiy[4]. Ni mtu anayetokana na ukoo wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Jina lake ni kama la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); Muhammad bin ´Abdillaah al-Mahdiy.

2 – Katika wakati wake atajitokeza ad-Dajjaal ambaye ataanza kudai kuwa ni mwema, kisha adai kuwa ni Mtume, kisha adai kuwa ni mungu. Ni mwenye chongo jicho lake la kulia.

3 – Kisha atateremka ´Iysaa mwana wa Maryam halafu amuue.

4 – Kisha atajitokeza Ya´juuj na Ma´juuj katika zama za ´Iysaa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Alama tatu hizi zitafuatana[5].

5 – Kisha zifuatane alama zingine za Qiyaamah. Miongoni mwa alama hizo ni moshi ambao utajaa mbinguni na ardhini. Moshi huo utampata muumini kama mafua ya kawaida na kafiri atapata maumivu makubwa[6].

6 – Kuondolewa kwa Qur-aan kutoka ndani ya misahafu na ndani ya vifua pale ambapo waislamu watapoacha kuitendea kazi[7].

7 – Kubomolewa kwa Ka´bah katika zama za mwisho[8].

8 – Mnyama ambaye atawaweka watu alama katika nyuso zao. Muumini atamuweka alama nyeupe na kafiri atamuweka alama nyeusi itayoufanya weusi uso wake[9].

9 – Miongoni mwa alama za mwisho ni kuchomoza kwa jua upande wa magharibi[10].

10 – Alama ya mwisho ya Qiyaamah miongoni mwa zile kumi ni moto utaotoka ndani ya Aden ambao utawafukuza watu katika uwanja wa mkusanyiko na ardhi ya Shaam. Moto huo utalala nao pindi watapolala na utalala nao mchana watapolala mchana[11]. Kisha baada ya hapo Allaah atatuma upepo mzuri kama harufu ya miski na ukiguswa ni kama hariri. Hautoacha nafsi yoyote ambayo ndani ya moyo wake kuna punde ya imani isipokuwa utaichukua. Kisha kutabaki juu yake watu waovu na Qiyaamah kitasimama juu yao[12].

Ulimwengu huu hautotokomezwa isipokuwa pale ambapo Tawhiyd na imani vitatoweka.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kisha akaondoka na tukatulia muda mrefu…. “

Kuna tamko lingine ya kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Mrudisheni.” Wakamfuata lakini hawakumpata yeyote. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee ‘Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza?” Tukasema: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Akasema: “Ilikuwa ni Jibriyl ambaye amekuja kuwafundisha dini yenu.”

[1] Muslim (648).

[2] at-Tirmidhiy (2210).

[3] al-Bukhaariy (5590).

[4] Abu Daawuud (4282).

[5] Muslim (2901).

[6] al-Bukhaariy (4774).

[7] Ibn Maajah (4049) na al-Haakim (8460) ambaye amesema:

”Hadiyth hii ni Swahiyh juu ya sharti za Muslim.”

[8] Ahmad (7910) na al-Haakim (8395) ambaye amesema:

“Hadiyth hii ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim na hawakuipokea.”

[9] al-Haakim (8490).

[10] al-Bukhaariy (4635) na Muslim (157).

[11] Ibn Maajah (4055).

[12] Muslim (1924).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 85-88
  • Imechapishwa: 14/02/2023