Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kisha akasema: “Nieleze kuhusu imani!” Akasema: “Ni kumuamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake na siku ya Mwisho na kuamini Qadar; ya kheri na ya shari yake.” Akasema: “Umesema kweli!” Akasema: “Nielezee kuhusu Ihsaan!” Akasema: “Ni kumuabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye Anakuona.” Akasema: “Nieleze kuhusu Qiyaamah.” Akasema: “Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.” Akasema: “Nieleze kuhusu alama zake!” Akasema: “Kijakazi kumzaa bibi yake na utaona wachunga wanaenda miguu chini, uchi na mafukara wakishindana kujenga majumba marefu.” Amesema: “Kisha akaondoka na tukatulia muda mrefu. Halafu akasema (Swallla Allaahu ´alayhi wa salalm): “Ee ‘Umar! Je, unamjua ni nani yule aliyekuwa akiuliza?” Nikajibu: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Akasema Mtume: “Ilikuwa ni Jibriyl ambaye amekuja kuwafundisha dini yenu.”

MAELEZO

Wakati alipohukumu maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ni kweli na ni kana kwamba anayasahihisha Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) wakashangazwa. Kwa sababu kikawaida muulizaji anakuwa hajui ilihali huyu anauliza ilihali anajua jibu na ndio maana akamsadikisha.

Maneno yake Mtume (´alayhis-Salaam):

“Muulizwaji si mjuzi kama asivyo vilevile muulizaji.”

Bi maana ujuzi wangu unalingana na ujuzi wako na mimi si mjuzi kukushinda. Kama ambavo wewe hujui basi nami pia sijui. Hakuna anayejua hilo isipokuwa Allaah:

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ۚ ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً

”Wanakuuliza kuhusu Saa ni lini kitatokea? Sema: ”Hakika ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha wakati wake isipokuwa Yeye. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haitokufikieni isipokuwa kwa ghafla.”[1]

Hakuna anayejua Qiyaamah isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Maneno yake Jibriyl (´alayhis-Salaam):

“Nieleze kuhusu alama zake!”

Bi maana nieleze kuhusu alama zinazojulisha juu ya kukaribia kwake. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamtajia alama mbili za kukaribia kwa Qiyaamah. Imesihi kutoka kwake, mbali na kwenye Hadiyth hii, alama nyinginezo nyingi.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kijakazi kumzaa bibi yake.”

Imekuwaje? Wanazuoni wamesema kuwa wafalme watashika na kuwa na wajakazi. Kwa maana nyingine masuria watakuwa wengi na hivyo wafalme wawafanye masuria. Matokeo yake kijakazi huyu amzae bibi yake kwa sababu ni msichana wa mfalme na hivyo awe ni bibi na bosi kwa mama yake au kwa wengine. Hivyo kijakazi aliyeachwa huru anakuwa amemzaa bibi yake. Imepokelewa katika baadhi ya mapokezi:

“Kijakazi kumzaa bwana wake.”[2]

Bi maana kijakazi amzae mwana wa mfalme na hivyo mtoto huyo awe mfalme kama baba yake. Kwa hiyo mwana huyo anakuwa ni bwana wa mama yake na wengine. Hilo litakuwa katika zama za mwisho.

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… na utaona wachunga wanaenda miguu chini, uchi na mafukara wakishindana kujenga majumba marefu.”

Bi maana watu wa mashambani ambao mara nyingi hawavai viatu. Nguo zao zinakuwa za kupasuka na haziwi kama za watu wa mijini. Kwa hivyo wanachunga wanyama hoa ambao wataendelea na kushindana kujenga majengo marefu baada ya kuwa walikuwa si wenye kuvaa viatu wala nguo. Walikuwa wakichunga kondoo. Wachunga hawa wenye kutembea peku na uchi, waliotajwa hapo kabla, wataishi katika miji mikubwa na watajenga majengo na majumba makubwa na marefu. Hii ni moja katika alama za Qiyaamah.

[1] 07:187

[2] al-Bukhaariy (50).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 84-85
  • Imechapishwa: 14/02/2023