Swali 57: Je, kutahadharisha mifumo inayoenda kinyume na walinganizi wake kunazingatiwa ni kuwagawanya waislamu na kuvunja umoja wao?

Jibu: Kutahadharisha mifumo inayopingana na mfumo wa Salaf kunahesabika ni kuwakusanya waislamu, si kuwagawanya. Kitu kinachogawanya umoja wa waislamu ni ile mifumo inayoenda kinyume na mfumo wa Salaf[1].

[1] Sunnah, kuisimamisha na kulingania kwayo hakujapatapo siku hata moja kufarikisha umoja wa waislamu. Kutahadharisha kutokana na Bid´ah na mapote na watu wake hakujapatapo pia kufarikisha umoja wa waislamu. Bali yote hayo yanahesabika ni kuwafanya wawe wamoja. Dalili juu ya hayo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa slalam) aliwatahadharisha Maswahabah na ummah wote kwa jumla juu ya Khawaarij.

Kuwanyamazia wazushi, mapote na wafuasi wao na mifumo yao ndio kunawagawanya waislamu. Wale wanaofanya hivo mara husema tusiwasengenye wanazuoni. Mara nyingine utawasikia wanasema kuwa nyama za wanazuoni zina sumu. Mara nyingine utawasikia wanasema kuwa tuache kuwashawishi watu. Mara nyingine utawasikia wakisema tusiwagawanye waislamu. Mara nyingine utawasikia wakisema badala yake tunapaswa kuwa na umoja dhidi ya adui yetu. Mara nyingine utawasikia wakisema maneno ya kipuuzi kwamba tunawaraddi ndugu zetu na tunawasalimisha makafiri, wanafiki, wanasekula na kadhalika. Wanayoyasema ni haki, lakini malengo yao ni batili. Bali misimamo kama hiyo ndio huwagawanya waislamu. Ingawa ukweli wa mambo hawa ndio adui wetu aliyeapishwa. Kwa sababu adui wa ndani ana khatari zaidi kuliko adui wa nje. Shaykh Abu Bakr Abu Zayd amesema:

”Wanazuoni wanao uwezo. Kila mmoja anakifanya kile anachokiweza kwa kutegemea uwezo wake. Wanasimama katika mipaka ya nchi na kuilinda kutokana na mashambulizi. Mwanachuoni mmoja anamraddi mkanamungu. Mwingine anamraddi mzushi mwepesi. Mwingine anamraddi mtenda dhambi. Mwingine anamraddi maoni dhaifu. Kila mmoja anafanya kulingana na uwezo na ustahili wake.” (ar-Radd ´alaal-Mukhaalif min Usuwl-il-Islaam, uk. 87)

Amesema tena:

”Kuwanyamazia wale wahalifu na kuwapuuza wale wanaorekebisha kuna mambo yanayoidhuru dini na dunia. Mosi ni Ahl-us-Sunnah kushuka ngazi na sambamba na hilo Ahl-ul-Ahwaa´ kuwa juu ya Ahl-us-Sunnah. Shubuha ikaenea na ikaingia ndani ya ´Aqiydah ya haki. ´Aqiydah ikawa inayumbayumba baada ya kwamba ilikuwa imara. Hivyo ´Aqiydah iliyosalimika ikanyongeka. Watu wa batili wakadhihiri katika mikusanyiko na juu ya mimbari. Kuvunja kizuizi kati ya Sunnah na Bid´ah, mema na maovu. Matokeo yake watu wakaburudika kwa batili na ile ghera ya dini ikafa. Baada ya hapo inakuwa vigumu kwa wanazuoni kuirekebisha jamii kwa sababu wanazikimbia mbali nasaha zao.” (ar-Radd ´alaal-Mukhaalif min Usuwl-il-Islaam, uk. 79)

Tunapendekeza kukisoma kitabu hiki.

Kuwaraddi Ahl-ul-Ahwaa´ wal-Bid´ah na kuwatahadharisha ni jambo lina matokeo mazuri. Bakr Abu Zayd (Rahimahu Allaah) amesema kuhusu kazi hii:

”Kusimamia wajibu huu kunafikiwa malengo mengi yaliyowekwa katika Shari´ah na matunda yaliyobarikiwa yanayong´aa katika maisha ya waislamu. Miongoni mwayo ni kuepukwa madhara yaliyotajwa punde yanayotokana na kunyamaza. Sunnah inaenezwa. Kuhuishwa kwa ille Sunnah iliyokwishakufa. Kama ambavo Sunnah inaenezwa kwa kule kuifanyia kazi na kulingania kwayo, vivyo hivyo inaenezwa kwa kurudisha yale mashambulizi juu yake, kumnasihi yule anayeenda kinyume na kusafisha uwanja kwa wale wanaoitwa wenye bahati mbaya ambao wanapingana na Qur-aan na Sunnah, wakazusha, wakatenda dhambi, wakaitupilia mbali Sunnah na kuwaudhi waislamu.” (ar-Radd ´alaal-Mukhaalif min Usuwl-il-Islaam, uk. 83)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 157-158
  • Imechapishwa: 24/03/2024
  • taaliki: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy