Miongoni mwa mambo yanayopaswa kuzingatiwa na kusisitizwa ni kuiheshimu Qur-aan, jambo ambalo baadhi ya wasomaji wanaokusanyika huyapuuza. Katika hayo ni kujiepusha na kucheka, kelele na mazungumzo wakati wa kisomo, isipokuwa maneno ya dharurah. Aidha atekeleze maneno yake (Ta´ala):

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ

“Inaposomwa Qur-aan basi isikilizeni na nyamazeni kimya ili mpate kurehemewa.”[1]

Afuate yale yaliyopokelewa na Ibn Abiy Daawuud:

”Wakati  Ibn ´Umar alipokuwa anasoma Qur-aan basi hakuwa akizungumza hadi amalize.”

Ameipokea al-Bukhaariy, ambaye amesema:

”Alikuwa hazumgumzi mpaka amalize.”

Hili limetajwa katika ”as-Swahiyh” katika kitabu kuhusu tafsiri ya Qur-aan katika mnasaba wa maneno Yake Allaah (Ta´ala):

نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ

“Wake zenu ni konde kwenu. Hivyo ziendeeni konde zenu vyovyote mpendavyo.”[2]

Katika hayo ni kuacha kuchezea mikono au kitu kingine, kwa sababu anazungumza na Mola wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa hivyo haifai kuchezea mbele Yake.

Vilevile kuacha kuangalia vitu vinavyomshughulisha na kuvuruga akili. Baya zaidi kuliko yote ni kuangalia yale ambayo hayaruhusiwi kuangaliwa, kama kijana asiye na ndevu na mfano wake. Kwa sababu kumtazama kijana mzuri bila haja ni haramu, ni mamoja iwe kwa matamanio au bila matamanio, ni mamoja iwe ana uhakika wa kutoingia kwenye fitina au hatokuwa na uhakika. Haya ndio maoni sahihi yaliyochaguliwa na wanazuoni. Imaam ash-Shaafi’iy (Rahimahu Allaah) na wanazuoni wengi wasioweza kuhesabika wameweka wazi juu ya uharamu wake. Dalili yake ni maneno Yake (Ta´ala):

قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ۚ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ

“Waambie waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao – hivyo ni utakaso zaidi kwao; hakika Allaah ni Mwenye khabari zote kwa yale wayatendayo. Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao.”[3]

Isitoshe kijana huyo yuko katika maana ya mwanamke, bali huenda baadhi yao au wengi wao wakawa wazuri zaidi kuliko wanawake wengi. Aidha sababu za shaka hupatikana kwake kwa urahisi na njia za shari zinakuwa rahisi kwake zaidi kuliko kwa mwanamke. Kwa hivyo kuharamishwa kwake kukawa na haki zaidi. Maneno ya Salaf katika kuwatahadharisha ni mengi yasiyohesabika, hata waliwaita “wachafu” kwa kuwa wanachukiza kwa mujibu wa Shari´ah. Ama kumtazama katika hali ya kuuza na kununua, kuchukua na kutoa, matibabu, kufundisha na mfano wa hayo katika hali ya haja, inaruhusiwa kwa dharurah. Hata hivyo anayemtazama ajikite kwenye kiwango cha haja tu na asizidishe kutazama bila dharurah. Na pia mwalimu anaruhusiwa tu kuangalia kiasi anachohitaji. Ni haramu kwa wote katika hali zote kuangalia kwa matamanio. Hili halihusiani tu na kijana asiye na ndevu, bali ni haramu kwa kila aliyebaleghe kuangalia kwa matamanio mtu yeyote, haijalishi kitu ni mwanaume au mwanamke, ni mamoja awe Mahram au asiye Mahram, isipokuwa mke au mtumwa anayemiliki halali ya kuburudika naye. Kiasi cha kwamba maswahiba wetu wamefikia kusema kwamba ni haramu kuangalia kwa matamanio hata maharimu kama dada au mama. Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

Ni juu ya wale wahudhuriaji katika kikao cha kisomo cha Qur-aan, pale wanapoona jambo lolote katika haya maovu yaliyotajwa au mengineyo, basi wanapaswa kulikataza kadiri ya uwezo kwa mkono kwa mwenye uwezo na kwa ulimi kwa asiyeweza kwa mkono lakini anaweza kuzungumza. Vinginevyo akemee kwa moyo wake. Allaah ndiye Mjuzi zaidi.

[1] 7:204

[2] 2:223 al-Bukhaariy (4526).

[3] 24:30-31

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 60
  • Imechapishwa: 02/09/2026