52. Nasaha za al-Khattwaab al-Makhzuumiy al-Qurashiy kwa mwanae III

1 – Usiondoshe unywele kutoka usoni mwako na wala usiondoshe nywele kutoka chini ya kidevu chako. Usikunekuke sana. Usiondoshe mvi. Usitie wanja mwingi. Usipindukie katika kuweka mafuta mengi kwenye nywele. Tia wanja siku moja na kuacha siku nyingine.

2 – Using´ang´ania mahitaji yako na wala usiyanyenyekee.

3 – Usimweleze mke wako, watoto wako wala mtu mwingine kiasi cha pesa zako. Wakiona ni ndogo, basi watakudharau. Wakiona ni nyingi, basi kamwe hutopata radhi zao. Watie khofu pasi na ghasia na kuwa mlaini kwao pasi na unyonge. Usifanye utani na wajakazi wako.

4 – Ukigombana basi unatakiwa kujiheshimu. Usiwe mkosefu wa adabu. Usiwe mwenye haraka. Zifikirie hoja zako.

5 – Hakikisha usiwe mwekundu usoni mwako na jasho katika paji la uso. Akiwepo mtu mwenye kukufanyia ujinga basi kuwa mpole. Pindi hasira zako zitapotulia ndipo uzungumze. Jiepushe na mambo ya ziada.

6 – Mtawala akisogea karibu nawe basi jitenge naye mbali kiasi cha mkuki. Akizungumza nawe kwa uzuri basi usijiaminishe kwamba hatokugeukia. Msifanyie upole kama unavomfanyia upole mtoto. Mzungumzishe yale anayotaka kusikia.

7 – Unapozungumza, basi sema kweli. Usinyanyue sauti kana vile unazungumza na mtu kiziwi. Usiishushe kama wale mabubu. Chagua maneno mazuri na zungumza mazungumzo mazuri. Usizungumze mambo ya ajabu yanayofanya mwili na ngozi kusisimka.

8 – Usiyarudirudi maneno. Usiseme “Ndio, ndio”, “Hapana, hapana”, “Wepesi, wepesi” na mfano wake.

9 – Usiwe mbadhirifu. Usiwe mtu wa hovyo. Hakikisha una utambuzi kwa yale yanayokupasa kwa pesa zako na utukufu wa rafiki yako. Usiwe mwenye kuwahitaji watu nao hawatokuhitaji.

10 – Mtu kutambua kiwango cha nafsi yake kunamtukuzia jina lake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 199-200
  • Imechapishwa: 20/08/2021