Allaah akiwaacha watu wamtape, wamsifu na wamtaje yule maiti kwa uzuri kunaweza kudhaniwa kwa nguvu kuwa mtu yule ni katika watu wema. Ni jambo lenye kuwezekana pindi Allaah anapompenda mja kuwafanya waislamu wakamtapa, wakamsifu na kumpenda. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَيَجْعَلُ لَهُمُ الرَّحْمَـٰنُ وُدًّا

“Hakika Mwingi wa Rahmah atajaalia mapenzi [tele kwa] wale walioamini na wakatenda mema.” 19:96

Imethibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi Allaah anapompenda mja humwita Jibriyl na kumwambia: “Allaah anampenda fulani nawe mpende.” Jibriyl akampenda. Kisha Jibriyl hunadi mbinguni: “Allaah anampenda fulani nanyi mpendeni.” Wakazi wa mbiguni humpenda na mtu yule akawa ni mwenye kukubalika ardhini.”

Tumeona hii leo na kufikiwa na khabari kutoka katika zama za wengine namna ambavyo wanachuoni, Ahl-ul-Hadiyth na wafanya biashara walivyosifiwa na kupendwa sana na watu. Maelfu ya watu walikuja kwenye mazishi yake. Pengine vilevile Allaah akazidisha ile idadi ya waliyoko pale kwa majini na Malaika. Huenda hata watu wakasikia ghasia kubwa kutoka upande wa mbinguni wakati wa kumzika. Shaykh wetu na ´Allaamah Shams-ud-Diyn Abul-Faraj ´Abdur-Rahmaan bin Muhammad al-Khatwiyb al-Maqdisiy amenieleza kwenye msikiti wa al-Mudhaffariy:

“Nilisikia ghasia hizi kutoka upande wa mbinguni mara nyingi kwa njia ya bishara njema… Marafiki zangu wengi wamenieleza namna na wao walivyozisikia wakati wa mazishi ya watu wema.”

Muhammad bin Yaziyd ar-Rifaa´iy amesema:

“´Amr bin Qays al-Malaa-iy alikufa katika upande wa kiajemi. Wakaja katika mazishi yake watu wasiohesabika idadi yao. Baada ya kumzika wakageuka na hakukuonekana yeyote.”

Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Watu walipita na jeneza na wakalisifu ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Imewajibika.” Kisha kukapita jeneza lingine ambalo wakalisema vibaya. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Imewajibika.” Ndipo ´Umar akasema: “Ee Mtume wa Allaah! “Watu wamepita na jeneza na wakalisifu ambapo ukasema: “Imewajibika.” na wakapita na jeneza lingine ambalo wakalisema vibaya na wewe ukasema: “Imewajibika.” ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Nyinyi ni mashahidi wa Allaah juu ya ardhi. Nyinyi ni mashahidi wa Allaah juu ya ardhi. Nyinyi ni mashahidi wa Allaah juu ya ardhi.”

Ameipokea al-Bukhaariy (1367) na Muslim (949).

Pindi Imaam Ahmad bin Hanbal alipokufa al-Haytham bin Khalaf alisema:

“Tulimzika Ahmad bin Hanbal siku ya ijumaa baada ya ´Aswr 241. Sijawahi kuona mkusanyiko mkubwa wa watu kama huo.”

Ibn Abiy Swaalih al-Qantwaariy amesema:

“Nimeshiriki katika majeneza kwa miaka 40 na sijawahi kuona jeneza la watu wengi kama hili.”

´Abdul-Wahhaab al-Warraaq amesema:

“Hatujui kuwa kumeshawahi kuwepo watu wengi katika jeneza katika kipindi cha washirikina na katika Uislamu kama katika mazishi ya Ahmad. Tumepata khabari kwamba walishiriki wanaume milioni moja na wanawake 60.000 – na wote wakishuhudia kwamba alikuwa mwema na walii.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Ukimuona mwanaume anafanya matendo mema na anasifiwa kwayo basi ujue kuwa hiyo ni bishara njema ya muumini inayokuja mapema.”

Wanachuoni wamesema bishara hii njema na ya mapema inathibitisha bishara yake njema Aakhirah. Allaah (Ta´ala) amesema:

بُشْرَاكُمُ الْيَوْمَ جَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Bishara njema [ni zenye kuwaelekea:] “Leo mabustani, yapitayo chini yake mito [ni yenye kukusubirini] na ni wenye kudumu humo! Huko ndiko kufuzu kuliko kukubwa!” 57:12

Bishara hii na ya mapema inathibitisha kuwa Allaah yuko radhi naye, anampenda na kwamba watu wanampenda.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 113-115
  • Imechapishwa: 22/10/2016