51. Bora kwa msafiri hii leo asifunge?

Swali 51: Ni lipi bora kwa msafiri aache kufunga au afunge na khaswa ikiwa ni safari isiyokuwa na uzito kama kusafiri na ndege au vyombo vyengine vya kisasa[1]?

Jibu: Bora kwa msafiri aache kufunga akiwa safarini kwa njia isiyofungamana. Atakayefunga hakuna neno juu yake. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumethibiti kutoka kwake yote mawili. Kadhalika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Lakini joto likiwa kali na kukawa kuna ugumu mkubwa basi kutasisitizwa zaidi kuacha kufunga na itakuwa imechukizwa kwa msafiri kufunga. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomuona mtu ambaye amefanyiwa kivuli safarini kutokana na ukali wa joto ilihali amefunga akasema:

“Sio katika wema kufunga safarini.”

Vilevile imethibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Hakika Allaah anapenda zitendewe kazi ruhusa Zake kama anavyochukia kuendewa maasi.”

Katika tamko lingine imekuja:

“… kama anavyopenda kutendewa kazi maamrisho Yake.”

Hakuna tofauti katika hayo baina ya yule mwenye kusafiri kwa gari, ngamia, safina, njia za bahari au ambaye anasafiri na ndege. Kwani yote hayo yamekusanya neno ´safari` na anatakiwa kutendea kazi ruhusa.

Allaah (Subhaanah) amewawekea waja Wake hukumu za safari na za ukazi wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallaam) na kwa wale wataokuja baada yao mpaka siku ya Qiyaamah. Hakika Yeye (Subhaanah) anajua yale yatayokuja kutokea katika kubadilika kwa hali na kuja aina mbalimbali za safari. Lau kungelikuwa kuna hukumu nyingine tofauti basi angeliibainishia Yeye (Subhaanah). Amesema (´Azza wa Jall):

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ

“Tumekuteremshia Kitabu kikiwa ni chenye kuweka wazi kila kitu na ni mwongozo na rehama na bishara kwa waislamu.”[2]

وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً ۚ وَيَخْلُقُ مَا لَا تَعْلَمُونَ

”Farasi na nyumbu na punda ili muwapande na wawe mapambo – na Anaumba msivyovijua.”[3]

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (15/237-238).

[2] 16:89

[3] 16:08

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Musaafir, uk. 67-69
  • Imechapishwa: 20/05/2022