48. Miongoni mwa alama kubwa zinazomfahamisha Allaah

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Miongoni mwa alama Zake ni usiku, mchana, jua na mwezi. Miongoni mwa viumbe Vyake ni mbingu saba na ardhi saba, vilivyomo ndani yake na vilivyomo kati yake.

MAELEZO

Miongoni mwa alama Zake… – Aayah zimegawanyika aina mbili:

1- Kuna alama za kilimwengu zinazoonekana. Kama mfano wa mbingu, ardhi, nyota, jua, mwezi, milima, miti na mawe. Zimeitwa kuwa ni ´alama` kwa sababu kupitia alama hizo zinamjulisha Muumbaji Wake (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwa ajili hiyo mshairi amesema:

Ajabu iliyoje ya kumwasi mungu    vipi anamkanusha mwenye kumkanusha

Ilihali katika kila kitu kuna alama    inayofahamisha kwamba ni Mmoja

Ni vipi mtu anaweza kumpinga Allaah (Jalla wa ´Alaa) na kusema kwamba hakuna Mola. Ulimwengu wote huu na viumbe vyote hivi vimepatikana pasi na Muumbaji? Ikiwa vimepatikana pasi po muumbaji, ni nani huyo muumbaji asiyekuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa)? Nibainishie? Huwezi kupata muumbaji asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ

”Au wamemfanyia Allaah washirika walioumba kama uumbaji Wake kisha yakafanana maumbile kwao?  “Sema: “Allaah pekee ni Muumbaji wa kila kitu, Naye ni Mmoja pekee, Aliyeshinda juu.”[1]

2- Alama za Qur-aan zinazosomwa kutoka katika Wahy uliyoteremshwa juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Zote hizi zinafahamisha juu ya uwepo wa Mola (Subhaanahu wa Ta´ala), ukamilifu Wake, sifa Zake, majina Yake na juu ya kwamba Yeye pekee, hali ya kuwa hana mshirika, ndiye anastahiki ´ibaadah. Zote hizi zinafahamisha hayo. Bi maana alama za kilimwengu na alama za Qur-aan.

Alama za kilimwengu zinafahamisha juu ya muumbaji na mwendeshaji wake. Alama za Qur-aan zimeamrisha kumwabudu Allaah, zimethibitisha Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, kuijulisha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na maamrisho ya kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Qur-aan yote inazunguka juu ya maana hii na imeteremshwa kwa ajili ya maana hii.

Miongoni mwa alama Zake ni usiku na mchana na jua na mwezi. Hizi ni miongoni mwa alama Zake kubwa (Subhaanahu wa Ta´ala). Usiku wenye giza unaofunika ulimwengu huu na mchana wenye kung´aa unaoangaza ulimwengu huu ambapo watu wakatapakaa kwa ajili ya kazi zao. Amesema (Ta´ala):

قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن جَعَلَ اللَّـهُ عَلَيْكُمُ اللَّيْلَ سَرْمَدًا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِضِيَاءٍ ۖ أَفَلَا تَسْمَعُونَ قُلْ أَرَأَيْتُمْ إِن جَعَلَ اللَّـهُ عَلَيْكُمُ النَّهَارَ سَرْمَدًا إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَنْ إِلَـٰهٌ غَيْرُ اللَّـهِ يَأْتِيكُم بِلَيْلٍ تَسْكُنُونَ فِيهِ ۖ أَفَلَا تُبْصِرُونَ وَمِن رَّحْمَتِهِ جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ لِتَسْكُنُوا فِيهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Sema: “Je, mnaonaje kama Allaah angelikufanyieni usiku ukaendelea daima mpaka siku ya Qiyaamah, nani mungu mwengine asiyekuwa Allaah atakayekuleteeni mwanga? – Je, kwa nini hamsikii?” Sema: “Je, mnaonaje kama Allaah angelikufanyieni mchana ukaendelea daima mpaka siku ya Qiyaamah, nani mungu asiyekuwa Allaah atakayekuleteeni usiku mpate utulivu ndani yake? – Je, kwa nini hamuoni?” Na kutokana na huruma Yake amekufanyieni usiku na mchana ili mpate utulivu ndani yake na ili mpate kutafuta sehemu ya fadhilah Zake na ili mpate kushukuru.”[2]

Usiku na mchana huu ni miongoni mwa alama Zake kubwa. Si kwamba kipindi chote inakuwa mchana au kipindi chote inakuwa usiku. Mambo yangelikuwa hivo basi kazi za watu zingeharibika. Allaah amewajaalia usiku na mchana kupishana. Usiku na mchana vimepangika; kimoja katika viwili hivyo hakichelewi na wala hakibadiliki. Vipo katika mpangilio mmoja. Ni miongoni mwa mambo yanayojulisha hekima ya Mwingi wa hekima (Subhaanahu wa Ta´ala). Pasi na kujali usanifu wa viundwa vya viumbe huchelewa na wakati mwingine kuharibika. Kuhusu viumbe vya Allaah (´Azza wa Jall) haviharibiki isipokuwa katika wakati ambao Allaah amepitisha viharibike. Usiku na mchana ni vyenye kuendelea. Hakuna chochote katika hivyo kinachovurugika. Upande wa pili viundwa vya viumbe huharibika na hukwisha ingawa ni vyenye nguvu au vikubwa. Ni mara ngapi mnaona wenyewe magari, ndege na meli zenye kutupwa pamoja na kwamba ni zenye nguvu na zimetunzwa lakini hata hivyo vinaharibika? Je, usiku au mchana umeshawahi kuharibika? Ni kwa sababu mtengenezaji wavyo ni Muweza na Mwingi wa hekima (Jalla wa ´Alaa):

صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ

“Utengenezaji wa Allaah ambaye ametengeneza kwa umahiri kila kitu.”[3]

[1] 13:16

[2] 28:71-73

[3] 27:88

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 104-107
  • Imechapishwa: 17/12/2020