Abu Ja´far at-Twahaawiy (Rahimahu Allaah) amesema:

77 – Waumini wote ni mawalii wa Mwingi wa huruma. Wabora wao mbele ya Allaah ni wale watiifu na wanaoifuata Qur-aan zaidi.

MAELEZO

Watu hao wameelezwa katika maneno Yake Allaah (Ta´ala):

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Tanabahi! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika. Ambao wameamini na wakawa wanamcha.”[1]

Haihusiani na kudai karama na mambo yasiyokuwa ya kawaida, kama wanavofikiria wengi. Bali mambo hayo ni katika utwevu ambao unachafua uzuri wa Uislamu.

Hapa kuna maashirio ya Radd kwa washupavu wa madhehebu ambao wanapendelea kuyafuata madhehebu na watu mbele ya Qur-aan na Sunnah. Kwa sababu hakuna uwiano wowote wa kufuata madhehebu na kufuata Qur-aan. Madhehebu ni yenye kutofautiana na Qur-aan na hakuna tofauti yoyote juu yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ ۚ وَلَوْ كَانَ مِنْ عِندِ غَيْرِ اللَّـهِ لَوَجَدُوا فِيهِ اخْتِلَافًا كَثِيرًا

“Je hawaizingatii Qur-aan? Na lau ingelikuwa imetoka kwa ghairi ya Allaah, bila shaka wangelikuta ndani yake khitilafu nyingi.”[2]

Kila ambavyo muislamu anakuwa mwenye kuifuata Qur-aan zaidi ndivo anavokuwa mkarimu zaidi mbele ya Allaah (Ta´ala). Na kila ambavo kunazidi kufuata kwake mchunga, ndivo anavyozidi kuwa kwake mbali. Hayo yameashiriwa na mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) pale aliposema:

”Hakuna anayefata kichwa mchunga isipokuwa mpumbavu au kipofu.”[3]

[1] 10:62-63

[2] 4:82

[3] Yamenakiliwa na ´Aabidiyn katika ”Rasm-ul-Muftiy” katika ”Majmuu´-ur-Rasaa-il” (1/32). Tazama ”Swifatu Swalaat-in-Nabiy”, uk. 41-43.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah – Sharh wa Ta´liyq, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 06/10/2024