47. ´Aqiydah ya Ibn ´Abdil-Wahhaab juu ya mitihani na neema za ndani ya kaburi


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Naamini mitihani ya ndani ya kaburi na neema zake.

MAELEZO

Hili ndio jambo la kwanza linalokuwa katika siku ya Mwisho. Maiti anapowekwa ndani ya kaburi lake, akamaliza kuzikwa, wakaenda zao waliomsindikiza na husikia nyayo za viatu vyao, anajiwa na Malaika wawili wakamkaza na roho yake ikarudishwa kwenye kiwiliwili chake. Hapo hupata uhai maalum wa ndani ya kaburi na sio kama uhai aliokuwa nao duniani. Uhai wa ndani ya kaburi hakuna aujuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Humuuliza: “Ni nani Mola wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume wako?” Muumini hujibu: “Mola wangu ni Allaah, dini yangu ni Uislamu na Mtume wangu ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu alikufa juu ya imani na hivyo atafufuliwa juu yake:

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya duniani na Aakhirah na Allaah huwaacha kupotoka madhalimu; na Allaah anafanya akitakacho.”[1]

Akijibu kwa majibu haya basi hunadi mwenye kunadi: “Amesema kweli mja wangu. Mtandikieni godoro kutoka Peponi, mfungulieni mlango wa Peponi, hukunjuliwa ndani ya kaburi lake kiasi cha upeo wa macho yake mpaka akaona nyumba yake Peponi na akafikiwa na upepo na harufu yake. Kaburi lake linakuwa ni bustani miongoni mwa mabustani ya Peponi. Husema: “Ee Allaah! Lete Qiyaamah ili nirudi kwa familia na mali zangu.

Kuhusu mnafiki ambaye alikuwa akiishi duniani juu ya shaka na akisema kwa mdomo wake kisichokuwemo ndani ya moyo wake akisema kwamba anashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, akisoma Qur-aan na akijifunza elimu na wakati huohuo ndani ya moyo wake hakuna imani. Anafanya mambo haya kwa sababu ya manufaa ya kidunia; ili aweze kuishi pamoja na watu ilihali si mwenye kuyaamini ndani ya moyo wake:

يَقُولُونَ بِأَفْوَاهِهِم مَّا لَيْسَ فِي قُلُوبِهِمْ

”Wanasema kwa midomo yao yale yasiyokuwemo katika nyoyo zao.”[2]

Huyu hatoweza kujibu ingawa duniani alikuwa amehifadhi vitabu, maisha, sarufi, tafsiri na Hadiyth zote. Katika kipindi hichi hatoweza kujibu muda wa kuwa hakuwa na imani. Kila atapoulizwa atasema: “Aah, aah, sijui! Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi pia nikakisema.” Bi maana mfano wa yale wanayosema watu bila kuyaamini ndani ya moyo wake. Alikuwa akiyasema kwa ajili ya kutaka kuwaridhisha watu. Ataambiwa: “Hukujua na wala hukusoma.”  Atapigwa rungu la chuma lau rungu hilo lingepigwa kwenye milima ya dunia basi ingelibomoka. Kisha atabanwa ndani ya kaburi lake mpaka mbavu zake zikutane. Kaburi lake liwe ni shimo moja wapo miongoni mwa mashimo ya Motoni. Aseme: “Ee Allaah! Usilete Qiyaamah!” Kwa sababu atajua kuwa yanayomsubiri baada ya kaburi ni makubwa zaidi. Atasema: “Ee Allaah! Usilete Qiyaamah!”

Haya ndio yatayokuwa ndani ya kaburi.

[1] 14:27

[2] 03:167

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 69-70
  • Imechapishwa: 07/04/2021