46. Radd ya nne juu ya makafiri wenye kupinga kufufuliwa


Jengine ni kwamba kungelikuwa hakuna kufufuliwa, hesabu na malipo basi ingepelekea watu kucheza na haki ya Allaah (Jalla wa ´Alaa) na kwamba anaumba viumbe ili wamalizike peke yake na maisha na matendo yao hayana natija yoyote. Amewaumba na kuwatunza. Miongoni mwako wako wanaofanya matendo mema na wanakufa na hawapati chochote katika malipo juu ya matendo yao. Miongoni mwao wako wanaofanya matendo maovu kama mfano wa maasi na ukafiri na wanakufa na hawapati chochote katika malipo juu ya matendo yao. Mambo yanaishilia namna hii? Hapana. Huku ni kutukana uadilifu wa Allaah (Jalla wa ´Alaa):

أَفَنَجْعَلُ الْمُسْلِمِينَ كَالْمُجْرِمِينَ مَا لَكُمْ كَيْفَ تَحْكُمُونَ

”Je, Tuwafanye waislamu sawa kama wahalifu? Mna nini nyinyi! Vipi mnahukumu?”[1]

Allaah hawafanyi waislamu kama wahalifu wote wakafa na hawapati chochote juu ya malipo ya matendo yao:

وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ۚ ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ أَمْ نَجْعَلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَالْمُفْسِدِينَ فِي الْأَرْضِ أَمْ نَجْعَلُ الْمُتَّقِينَ كَالْفُجَّارِ

“Hatukuumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake pasipo malengo – hiyo ndio dhana ya wale waliokufuru; basi ole wale waliokufuru kwa moto utakaowapata. Je, Tuwajaalie wale walioamini na wakatenda mema kama wenye kueneza ufisadi ardhini au tuwajaalie wachaji kama waovu?”[2]

Hakuna kufufuliwa na kulipwa. Mfanya mema halipwi juu ya mema yake na mfanya mabaya halipwi juu ya mabaya yake. Huu ni mchezo kwamba Allaah awaumbe viumbe na awaache na kusiwe na matokeo yoyote na wafanye matendo maovu au matendo mema na kusiwe na matunda wala matokeo yoyote. Huu ni mchezo na ni kutukana uadilifu wa Allaah (Jalla wa ´Alaa):

أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ

“Je, mlidhania kwamba Sisi tulikuumbeni bila kusudio na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?” Ametukuka Allaah mfalme wa haki [ambaye] hapana mungu wa haki ila Yeye. Mola wa ‘Arshi tukufu.””[3]

Allaah (Ta´ala) ametakasika kutokamana na hayo kwamba amewaumba viumbe hawa na akawaacha wakafa na matendo yao yasiwe na natija yoyote na muumini asipambanuke kutokamana na kafiri. Bali pengine kafiri huyu akawa ni mwenye kustareheshwa katika dunia hii ilihali yuko katika maasi na ukafiri na muumini katika maisha haya ya duniani akawa na maisha magumu na asipate chochote katika malipo yake. Haya yanapelekea kutukana uadilifu wa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Kadhalika yanapelekea kwamba amewaumba viumbe bure na hakuna natija yoyote juu ya matendo yao. Huku ni kutukana hekima na uadilifu wa Allaah (Jalla wa ´Alaa).

Kwa hivyo hizi ni miongoni mwa dalili za kufufuliwa ambazo Allaah amezitaja ndani ya Qur-aan tukufu katika sehemu mbalimbali. Kuamini kufufuliwa ni nguzo miongoni mwa zile nguzo sita za imani. Ni jambo limetajwa kwa kukariri katika Qur-aan tukufu.

[1] 68:35-36

[2] 38:27-28

[3] 23:115-116

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 67-69
  • Imechapishwa: 07/04/2021