48. Ulazima wa kuamini adhabu na neema za kaburi na ukafiri wa anayeyapinga


Kuamini adhabu za kaburi au neema zake ni jambo la lazima. Kwa sababu ni jambo ambalo dalili zake zimetajwa kwa wingi ndani ya Qur-aan na Sunnah[1]. Ni lazima kuamini adhabu na neema za ndani ya kaburi. Mwenye kupinga kwa kukusudia ni kafiri. Ama akiwa ni mwenye kufuata kichwa mchunga au mwenye kupindisha maana ni mpotevu. Lakini mwenye kupinga kwa kukusudia baada ya kujua ni kafiri.

Ni jambo limepingwa na Mu´tazilah wenye kutumia akili. Kwa sababu wanategemea akili zao na wanasema kuwa endapo tutafukua kaburi tutalikuta kama tulivyoliweka; ndani yake hakuna Pepo wala Moto. Tunawajibu kwa kusema: nyinyi mko katika ulimwengu wa dunia na yeye yuko katika ulimwengu wa Aakhirah. Adhabu au neema zinamjia pasi na nyinyi kuhisi jambo hilo. Kwa sababu hayo ni miongoni mwa mambo ya Aakhirah ambayo hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na wala akili hazina upeo wa kuyaelewa mambo hayo. Kinachotegemewa ni zile nukuu zilizosihi na khabari zikapokelewa kwa mapokezi mengi. Kwa hiyo tunayaamini na wala hatuyapekui. Kwa sababu haya ni miongoni mwa mambo yaliyofichikana ambayo hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Wewe unaweza kuwaona watu hivi sasa ambapo baadhi yao wako katika furaha na raha na wengine wako katika msongo wa mawazo na mahuzuniko na wakati huohuo wote wanatembea, wanakula na wanakunywa na wewe hujui hali ya mmoja kutokamana na mwengine; humjui ni nani mwenye furaha na ni nani asiyekuwa na furaha. Kwa sababu haya ni mambo yaliyojificha ambayo hakuna ayajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Maneno yake:

“Naamini mitihani ya ndani ya kaburi na neema zake.”

Fitina za kaburi bi maana mitihani. Kwa sababu atajiwa na watoaji wawili wa mitihani ambao ni Malaika wawili wamuulize na wampe mitihani.

[1] al-Bukhaariy (1374, 1337), Muslim (2870) kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh). Pia imepokelewa kupitia kwa Abu Hurayrah, Jaabir, ´Aaishah, al-Baraa´ na Abu Sa´iyd (Radhiya Allaahu ´anhum). Tazama ”Fath-ul-Baariy” (03/237-238).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 07/04/2021