46. Uwajibu wa kuisoma na kuielewa Qur-aan kwa mujibu wa Salaf

Allaah (Ta´ala) ametuneemesha kwa Kitabu Chake ambacho amekifanya ni chenye kubainisha kila kitu na ni uongofu, rehema na bishara njema kwa Waislamu. Mtu wa batili hawezi kuja na hoja isipokuwa katika Qur-aan kuna yanayoivunja na kubainisha ubatilifu wake. Kama alivyosema (Ta´ala):

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

”Na wala hawatakujia kwa mfano wowote ule, isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri bora kabisa.” (al-Furqaan 25 : 33)

Wamesema baadhi ya wafasiri, Aayah hii ni jumla kwa kila hoja ambayo watakuja nayo watu wa batili mpaka siku ya Qiyaamah.

MAELEZO

Hii ni kanuni yenye kujulikana kwa kuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema kuhusu Qur-aan:

تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ

“Kinachoweka wazi kila kitu.” (16:89)

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا

”Na wala hawatakujia kwa mfano wowote ule, isipokuwa Tunakuletea haki na tafsiri bora kabisa.” (25:33)

Hakuna utata au batili duniani inayoletwa na kafiri au mkanamungu isipokuwa katika Qur-aan kuna kinachokirudi. Hata hivyo haya hayawezi kubainika isipokuwa kwa kuitambua Qur-aan, kuielewa na kuisoma ukweli wa kuisoma mpaka mtu aweze kujua ile hazini, silaha na risasi zinazopatikana ndani yake kwa ajili ya kukabiliana na maadui wetu. Kwa hivyo tuikimbilie Qur-aan – kwa kuihifadhi, kuielewa, kuisoma, kuizingatia na kuitendea kazi – ili tuwe ni wenye silaha walio tayari. Ama Qur-aan kuwa kwetu tu pasi na kuitilia umuhimu na kuisoma haitoshi. Ahl-ul-Kitaab wamepotea na wakakufuru ilihali wako na Tawraat na Injiyl pindi walipoacha kujifunza na kuvitendea kazi viwili hivyo.

Lakini hata hivyo ni lazima kuisoma Qur-aan chini ya kivuli cha Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuifasiri kwa mujibu wa Salaf-us-Swaalih na sio kwa mujibu wa masomo ya sasa yaliyojengwa juu ya papara, ujinga au yale wanayoita kuwa ni miujiza ya kiyasansi. Namna hii ya kutangamana na Qur-aan sio maalum kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au watu wa wakati wake. Hili ni kwa watu watu wote mpaka pale Qiyaamah kitaposimama. Lakini hata hivyo inatakiwa kuitilia umuhimu Qur-aan na kuisoma kama ipasavyo. Ndani yake inabainisha haki na kuwaraddi watu wa batili.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 64
  • Imechapishwa: 18/12/2016