Mja anatakiwa pindi atapoona au kusikia yale tuliyotangulia kuyataja katika mlango huu na namna kulivyo aina mbalimbali za kufa shahidi, kuliwazika kwa kufa kipenzi chake. Mara nyingi yule aliyekufa hupata kitu katika hayo yaliyotajwa ingawa sikusoma kila kilichothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu kufa shahidi. Imepokelewa ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kifo cha kigeni ni kufa shahidi.”[1]

Nimetaja vya kutosha kuhusu kufa shahidi katika kitabu “Ahkaam-ut-Twaa´uun”. Hadiyth iliyopokelewa na Ahmad inatosha kuwa bishara njema:

“Mashahidi wengi wa Ummah wangu ni wale wanaokufa kitandani.”[2]

Kumeshatangulia yale wanayolipwa mashahidi wakati wa kufa na ule ujira unaowasubiri mbele ya Allaah na namna roho zao zilivyo kwenye ndege wa kijani wanaokula, kunywa na kuruka wanavyotaka Peponi. Yote haya yanapitika katika maisha ya ndani ya kaburi. Pindi baadaye wanapoingia Peponi kwa viwiliwili vyao watahama kwenda katika neema kubwa na ilio bora zaidi. Abu Bakr al-Qaatw´iy amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wake kwamba kuna mwanamke alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Ni nani yuko Peponi?” Akasema: “Mtume yuko Peponi, shahidi yuko Peponi, mtoto mchanga mwenye kuzaliwa yuko Peponi na mtoto mchanga mwenye kuzaliwa aliyezikwa akiwa hai yuko Peponi.”[3]

Mja kuhama kwenda kwa Allaah ni bora na yale yaliyo kwa Allaah ni bora kwake kuliko kubaki katika dunia hii na vile alivyoumbiwa kwavyo. Anawatazama namna wanavyotenda. Anawapa mtihani kwa matatizo, majanga na kufa shahidi ili aweze kujua ni nani mwenye kusubiri na ni nani mwenye kukata tamaa ili aweze kumlipa kila mmoja kutokana na alivyotenda. Kuna wenye kulipwa kwa mabustani na kuna wengine wenye kulipwa kwa Moto. Hamdhulumu yeyote kabisa. Akimwingiza mtu Peponi basi ni kutokana na huruma na fadhila Zake na akimwingiza mtu Motoni ni kutokana na uadilifu na nguvu Zake:

لَا يُسْأَلُ عَمَّا يَفْعَلُ وَهُمْ يُسْأَلُونَ

“Haulizwi kwa yale Anayoyafanya lakini wao wataulizwa.” 21:23

Himdi zote anastahiki Allaah kwa kila hali.

[1] Dhaifu kwa mujibu wa Ibn-ul-Jawziy katika ”al-´Ilal al-Mutanaahiyah”.

[2] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilat-ul-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” (2988).

[3] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Swaghiyr-il-Jaami´” (5997).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 228
  • Imechapishwa: 20/12/2016