Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

اهدِنَا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoze katika njia iliyonyooka… ”[1]

Yaani tuongoze, utuelekeze na ututhibitishe. Njia ni Uislamu. Imesemekana pia kuwa ni Mtume na wengine wakasema kuwa ni Qur-aan. Maana zote hizi ni haki. Iliyonyooka ni ile ambayo isiyokuwa na upindaji wowote ndani yake.

MAELEZO

Hii ni Aayah ya tano. Tuongoze katika njia ilionyooka. Tuongoze na tuelekeze kwa yale tusiyoyajua na pia ututhibitishe kwa yale tunayoyajua na utujaalie kuyatendea kazi. Kwa sababu yapo mambo katika haki usiyoyajua na wala huyajui. Kwa hiyo unamwomba Mola wako akuongoze na akuelekeze kwayo. Yapo mambo ambayo umeyajua na umeyafanyia kazi na hivyo unamwomba Allaah akuthibitishe juu yake. Yapo mambo ambayo umeyajua lakini hujayafanyia kazi na hivyo unamwomba Allaah akuwafikishe kwayo. Yote haya yanaingia katika maneno yako unaposema:

اهدِنَا

“Tuongoze… ”

Maneno yake:

الصِّرَاطَ

“… njia… ”

Njia ni Uislamu. Imesemekana pia kuwa ni Mtume na wengine wakasema kuwa ni Qur-aan.”

Kuna maoni matatu:

1 – Uislamu.

2 – Mtume.

3 – Qur-aan[2].

Maneno yake:

“Maana zote hizi ni haki.”

Yule ambaye atanyooka juu ya dini ya Uislamu atakuwa juu ya njia ilionyooka. Yule mwenye kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atakuwa juu ya njia ilionyooka. Yule mwenye kuitendea kazi Qur-aan atakuwa juu ya njia ilionyooka. Maana zote ni haki na wala hakuna mgongano kati yazo.

Maneno yake:

المُستَقِيمَ

“… iliyonyooka… ”

Ni ile ambayo isiyokuwa na upindaji wowote ndani yake.”

Makusudio ya njia hii ni ya kimaana. Nako ni kule kulazimiana na haki.

Ipo pia njia ya kuhisiwa siku ya Qiyaamah. Ni njia ambayo itawekwa juu ya Moto wa Jahannam. Ni daraja itakayokuwa kati ya Pepo na Moto ambayo watu watapita juu yake kutegemea na matendo yao. Kwa hiyo zipo njia mbili; njia duniani na njia huko Aakhirah. Ambaye atanyooka juu ya njia ilionyooka duniani basi atavuka njia ya kuhisiwa siku ya Qiyaamah mpaka kuingia Peponi. Ambaye hatonyooka juu ya njia ilionyooka duniani basi hatovuka njia yenye kuhisiwa siku ya Qiyaamah na hivyo atatumbukia Motoni.

Maneno yake:

اهدِنَا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoze katika njia iliyonyooka… ”

Du´aa ambayo ni tukufu, yenye manufaa zaidi na yenye kukusanya zaidi ipo katika al-Faatihah. Mtu anahitajia du´aa hii na uongofu zaidi kuliko anavohitajia kula na kunywa. Bali ni kukubwa zaidi kuliko anavohitajia kupumua. Kwa sababu mtu akikosa chakula na kinywaji atakufa, jambo ambalo ni lazima tu litamfika karibuni au huko baadaye. Haina neno mtu akifa muda wa kuwa ni mwenye kunyooka katika kumtii Allaah na anamwabudu Yeye pekee. Lakini mtu akikosa kuongozwa basi inakufa roho na moyo wake na hivyo anaingia Motoni. Kwa hiyo ndio maana ikawa kukosa kuongozwa kukawa ni kubaya zaidi kuliko kukosa chakula, kinywaji na kupumua.

[1] 01:06

[2] Tazama ”Tafsiyr Ibn Kathiyr” (01/28,29).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 76-78
  • Imechapishwa: 20/06/2022