Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

صِرَاطَ الَّذِينَ أَنعَمتَ عَلَيهِمْ

”… njia ya wale uliyowaneemeshe.”[1]

Njia ya wale uliyowaneemeshe. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”[2]

MAELEZO

Hii ndio tafsiri ya njia ilionyooka. Hii ndio njia ya wale walioneemeshwa.

اهدِنَا الصِّرَاطَ المُستَقِيمَ

“Tuongoze katika njia iliyonyooka… ”

Bi maana, ee Allaah, tuongoze njia ilionyooka ambayo ni Uislamu na yale yaliyokuja ndani ya Qur-aan tukufu na yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hii ndio njia ya wale walioneemeshwa kwa elimu na matendo. Allaah amewatunuku elimu na hivyo wakaijua haki. Kisha Allaah akawatunuku na hivyo wakaitendea kazi.

Maneno yake:

Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَمَن يُطِعِ اللّهَ وَالرَّسُولَ فَأُوْلَئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللّهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاء وَالصَّالِحِينَ وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

“Atakayemtii Allaah na Mtume basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah aliowaneemesha – Manabii na wakweli na mashahidi na waja wema – na uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”

Kuna watu sampuli nne ambao Allaah amewaneemesha:

1 – Mitume.

2 – Wakweli.

3 – Mashahidi.

4 – Waja wema.

وَحَسُنَ أُولَئِكَ رَفِيقًا

”Uzuri ulioje kuwa na tangamano kama hili!”

Kwa kukusanyika nao Peponi na kuliwazika kwa kuwa karibu nao jirani na Mola wa walimwengu. Hawa ndio walioneemeshwa na Allaah kwa elimu na matendo. Wao ndio wako juu ya njia ilionyooka. Kwa hivyo wewe unamwomba Allaah akuongoze njia ilionyooka ambayo ndio njia ya watu hawa.

Wanaoshika nafasi ya mbele kabisa ni Mitume ambao Allaah amewaneemesha unabii na ujumbe.

Kisha wanafuatiwa na wakweli. Ni yule ambaye imekuwa na nguvu imani yake na kusadikisha kwake mpaka imani yake ikachoma moto mambo ya utata na ya matamanio kaisi cha kwamba akawa hayaendei maasi. Katika kilele chao anakuja yule as-Swiddiyq mkubwa; Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh).

Kisha wanafuatiwa na mashahidi. Shahidi ni yule anayeuliwa katika uwanja wa vita kwa ajili ya kulinyanyua juu neno la Allaah. Amejitolea nafsi yake ilioko kati ya mbavu zake – ambayo ndio kitu kitukufu zaidi anachomiliki mtu – akaifanya rahisi kwa ajili ya kulinyanyua neno la Allaah na hivyo roho yake ikahamishwa kupelekwa Peponi.

Kuhusu ambaye anapiga vita kwa ajili ya hasira tu, kwa kujionyesha na utaifa ni batili na si kwa ajili ya Allaah. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Muusa (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema: ”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu mtu ambaye anapigana vita kwa ajili ya ushujaa, mori au anapigana vita kwa kujionyesha – ni nani katika hao ambaye yuko katika njia ya Allaah? Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

”Yule ambaye anapigana vita ili neno la Allaah liweze kuwa juu ndiye yuko katika njia ya Allaah.”[3]

Kisha wanafuatiwa na waja wema. Hawa ni wale ambao yametengemaa matendo yao na yamefanywa kwa ajili ya Allaah pekee na kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 01:07

[2] 04:69

[3] al-Bukhaariy (123) na Muslim (1904).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 78-81
  • Imechapishwa: 20/06/2022