Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

2 – Msingi wa pili:

Ni kuijua dini ya Kiislamu kwa dalili. Nako ni kujisalimisha kwa Allaah kwa Tawhiyd, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga mbali na Shirki na watu wake. Hili lina daraja tatu: Uislamu, imani na ihsaan. Kila daraja ina nguzo zake.

Ngazi ya kwanza: Uislamu una nguzo tano: Kushuhudia ya kwamba hapana mungu anayeabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji Nyumba ya Allaah tukufu.

MAELEZO

Baada ya mja kumtambua Mola wake, ambaye ni Allaah, kunafuatia msingi wa pili ambao ni kuujua Uislamu. Ni lazima kwako kuujua Uislamu kwa dalili. Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amekutambulisha Uislamu ya kwamba ni kule kujisalimisha kwa Allaah kwa kumpwekesha, kunyenyekea Kwake kwa kumtii na kujitenga mbali na shirki na watu wake.

Kujisalimisha maana yake ni kunyenyekea, kujidhalilisha na kutii. Husemwa kwamba ngamia amejisalimisha kwa mwenye naye wakikusudia kwamba amenyenyekea na amemwongoza kwa kamba yake. Kwa hivyo yule mwenye kujisalimisha amenyenyekea[1]. Ambaye hajisalimishi ndiye ambaye huitwa kuwa ni mwenye kufanya kiburi. Muislamu anajisalimisha kwa Allaah kwa njia ya kwamba ananyenyekea Shari´ah na dini Yake. Kafiri ni mwenye kufanya jeuri, kiburi na amekataa kurejea kwa Allaah na hivyo akawa mwenye kufanya kiburi.

1 – Ngazi ya Uislamu, nayo iko chini.

2 – Ngazi ya imani, nayo iko juu kushinda ya kwanza.

3 – Ngazi ya ihsaan, nayo iko juu zaidi kushinda hizo mbili.

Kisha mtunzi (Rahimahu Allaah) akaanza kubainisha kila moja katika ngazi hizo tatu.

[1] Tazama ”Lisaan-ul-´Arab” (12/293).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 70-71
  • Imechapishwa: 12/02/2023