Jahmiyyah wanadai kuwa jina la Allaah (´Azza wa Jall) ndani ya Qur-aan ni kiumbe. Tukawauliza alikuwa anaitwa nini kabla ya kuumba jina hilo, wakajibu kwamba hakuwa na jina lolote. Ndipo tukasema kwamba basi vivyo hivyo alikuwa ni mjinga kabla ya kujiumbia elimu Yake, alikuwa hana nuru kabla ya kujiumbia nuru Yake, alikuwa hana uwezo kabla ya kujiumbia uwezo Wake. Ndipo mbaya huyu akajua kuwa Allaah amemfedhehesha na kumfichua pale alipodai kuwa jina la Allaah (´Azza wa Jall) ndani ya Qur-ana limeumbwa.

Tukawaambia Jahmiyyah endapo mtu ataapa kwa kusema uwongo kwa jina la Allaah ambaye hakuna mungu wa haki mwingine isipokuwa Yeye, basi hatotakiwa kutoa kafara ya kiapo chake kwa sababu ameapa juu ya kitu kilichoumbwa na hakuapa kwa Muumba. Aidha Allaah akamfedhehesha kwa hilo pia. Vilevile tukamuuliza kwamba si alikuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr, ´Umar, ´Uthmaan, ´Aliy na makhaliyfah, watawala na mahakimu walikuwa wakiwataka watu kuapa kwa jina la Allaah ambaye hakuna mungu wa haki mwingine asiyekuwa Yeye? Hiyo ina maana kuwa walikuwa wakifanya makosa; badala yake ilitakiwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wale waliokuja baada yake wawatake watu waape kwa Yule ambaye anaitwa Allaah. Vilevile walitakiwa kusema ambaye anataka kusema hakuna mungu wa haki mwingine asiyekuwa Allaah, basi waseme hapana mungu wa haki isipokuwa yule aliyeumba. Vinginevyo haitosihi Tawhiyd yao. Hivyo Allaah akawafedhehesha kutokana na ule uwongo waliyomsemea Allaah. Lakini sisi tunasema kuwa Allaah ni Allaah. Allaah si kitu kingine isipokuwa jina. Majina ni kitu kingine kisichokuwa Allaah. Allaah amewaumba viumbe kwa kitu gani ikiwa hazungumzi?

Wanauliza kama ipo dalili juu ya kwamba Allaah amewaumba viumbe kauli na maneno Yake. Ndio, amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا قَوْلُنَا لِشَيْءٍ إِذَا أَرَدْنَاهُ أَن نَّقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

”Hakika hapana vyengine neno Letu juu ya jambo Tunapokitaka tunakiambia: “Kuwa!” – basi kinakuwa.”[1]

Wanasema maana ya Aayah ni kwamba mambo mara moja yanakuwa pale tu Anapotaka. Tulipowauliza ni kwa nini wamebagua ”Kuwa!”, wakasema kuwa kila kitu ndani ya Qu-aan kina maana yake. Allaah kusema, ni kama waarabu wanavosema ukuta unazungumza au mtende unazungumza, ambapo ukaanguka. Tukawauliza Allaah aliwaumba viumbe kwa kitu gani kwa vile nyinyi miongoni mwa ´Aqiydah yenu ni pamoja na kwamba Allaah hazungumzi. Wakajibu kwamba ni kwa uwezo Wake. Tukawauliza kama ni kitu.  Wakajibu kwa kuitikia ndio. Ndipo tukawauliza kama aliumba uwezo huo pamoja na vitu vyengine vilivyoumbwa. Wakajibu kwa kuitikia ndio. Ndipo tukasema ni kama kwamba Ameumba kiumbe kwa kiumbe kingine. Hivyo mmepingana na Qur-aan pale Allaah (Ta´ala) aliposema:

لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

”Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye Muumbaji wa kila kitu.”[2]

Allaah akatueleza kwamba Yeye ndiye anaumba. Amesema tena:

هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ

”Je, kuna muumbaji mwingine badala ya Allaah anayekuruzukuni kutoka mbinguni na kwenye ardhi?”[3]

Hakuna mwengine zaidi Yake anayeumba. Pia mmedai kuwa kuna mwingine asiyekuwa Yeye anayeumba viumbe. Ametakasika Allaah kutokana na yale wanayoyasema Jahmiyyah kutakasika kukubwa[4]!

[1] 16:38

[2] 6:102

[3] 35:3

[4] Ibn ´Aqiyl al-Hanbaliy amesema:

”Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ameandika kitabu kinachoitwa ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah wal-Qadariyyah.” (al-Aadaab ash-Shar´iyyah (1/274))

Ibn Taymiyyah amesema:

”Kama alivosema Imaam Ahmad katika kitabu chake ”ar-Radd ´alaaz-Zanaadiqah wal-Jahmiyyah.”  (Tafsiyr Suurat-il-Ikhlaasw, uk. 239)

Ibn Kathiyr amesema:

”… na hivo ndivo alivosema Ahmad bin Hanbal katika kitabu ”ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah” (Tafsiyr al-Qur-aan al-´Adhwiym (3/304))

Ibn Hajar al-´Asqalaaniy amesema:

”Amesema waziwazi Ahmad katika kitabu “ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah.” (Fath-ul-Baariy (13/598))

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 162-165
  • Imechapishwa: 30/04/2024