Swali: Nauliza kuhusu usomaji wa Qur-aan na kukaa msikitini kwa yule mwenye hedhi, mwenye janaba na kusikiliza Dhikr msikitini. Kwa sababu kumepokelewa baadhi ya Hadiyth na mapokezi. Miongoni mwazo ni Hadiyth ya ´Aaishah wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipomwambia ampokeze kitambara ambapo ´Aaishah akamweleza kwamba yuko na hedhi. Akamwambia:

”Hedhi yako haiko mikononi mwako.”

Hadiyth nyingine inasema:

”Fanya yale yote anayofanya mwenye kutufu.”

na wala hakumwambia asiingie msikiti Mtakatifu. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiegemea juu ya mapaja yake [Aaishah wakati wa hedhi]. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimdhukuru Allaah katika hali zake zote. Maswahabah zake walikuwa wakilala msikitini na wakipatwa na janaba ndani yake. Tunaomba kuwekewa wazi dalili hizi.

Jibu: Kuhusu jambo la kukaa msikitini si halali kwa mwenye hedhi kukaa msikitini. Haijalishi kitu ametia wudhuu´ au hana wudhuu´. Dalili ya hilo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimkataza ´Aaishah kufanya Twawaaf kwenye Ka´bah kwa sababu kufanya Twawaaf kutampelekea kukaa.

Kuhusu Hadiyth ya kumpokeza kitambara ifahamike kwamba kumpelekea kitambara msikitini sio kukaa msikitini. Bali ni kupita tu ndani yake. Inafaa kwa mwenye hedhi kupita msikitini ikiwa kutaaminika kuwa hatochafua.

Kuhusu mwenye janaba haifai kwake kukaa msikitini isipokuwa mpaka atie wudhuu´. Maswahabah waliokuwa wakilala msikitini, tuna haki ya kukuuliza: ni nani aliyekwambia kwamba walikuwa wakifanya hivo wakati wa janaba? Wakipatwa na janaba wakati wamelala, basi ifahamike kwamba mwenye kulala hapati dhambi. Wakiamka wudhuu´ unawatosha. Kwa sababu inafaa kwa mwenye janaba kukaa msikitini akitawadha.

Kuhusu kusoma Qur-aan, ifahamike kuwa si halali kwa mwenye janaba kusoma Qur-aan mpaka aoge kwanza. Mwenye hedhi inafaa kwake kusoma Qur-aan wakati wa haja au kukiwa kuna manufaa ya kufanya hivo. Haja ni kwa mfano anasoma Qur-aan ili asiisahau, anasoma Qur-aan kwa ajili ya kumfunza mtoto wake, mwalimu anayewafunza wasichana, ni mwanafunzi wa kike anayetaka kumsikilizisha mwalimu wake na mengineyo. Yote haya hayana neno. Ama kusoma kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah lililo salama zaidi ni yeye kutofanya hivo. Kwa sababu wanachuoni wengi wanaonelea kwamba haifai kwake kusoma Qur-aan. Yeye si mwenye haja ya kufanya hivo. Hivyo akisoma Qur-aan kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah kwa kisomo hicho atakuwa ni mwenye kuzunguka kati ya madhambi na thawabu. Ni mwenye kupata dhambi kwa mtazamo wa baadhi ya wanachuoni na ni mwenye kupata thawabu kwa mtazamo kwa wanachuoni wengine. Lililo bora ni salama.

Kwa kufupiza ni kwamba inafaa kwa mwenye janaba kukaa msikitini akitawadha. Si halali kwa mwenye janaba kusoma Qur-aan kwa hali yoyote. Kwa sababu jambo liko mikononi mwake; anaweza kuamua kuoga na kusoma Qur-aan. Haijuzu kwa mwenye hedhi kukaa msikitini kabisa na inafaa kwake kupita. Inajuzu kwa mwanamke mwenye hedhi kusoma Qur-aan kwa sababu ya haja au maslahi fulani.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (377) http://binothaimeen.net/content/13364
  • Imechapishwa: 07/10/2020