Kuhusiana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“… kuamrisha mema ni swadaqah na kukataza maovu ni swadaqah.”[1]

Kuamrisha mema na kukataza maovu ni miongoni mwa swadaqah zilizo bora kabisa. Allaah ameufadhilisha Ummah huu juu ya nyumati zingine kwa jambo hili. Allaah (Ta´ala) amesema:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa ulioteuliwa kwa watu – mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.” (03:110)

Lakini hata hivyo jambo la kuamrisha mema na kukataza maovu ni lazima liwe na sharti zifuatazo:

1 – Yule mwenye kuamrisha na kukataza awe ni mjuzi wa hukumu ya Kishari´ah. Haijuzu kwake kuzungumza ikiwa ni mjinga. Yule anayeamrisha mema na kukataza maovu anawaamuru watu kwa yale ambayo anaamini kuwa ndio Shari´ah ya Allaah. Hafai kuzungumza juu ya Shari´ah ya Allaah kwa mambo asiyoyajua. Allaah ameharamisha hilo. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ وَالْإِثْمَ وَالْبَغْيَ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَأَن تُشْرِكُوا بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ سُلْطَانًا وَأَن تَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ

“Sema: “Hakika hapana vyengine Mola wangu ameharamisha machafu yote yaliyodhihirika na yaliyofichika na dhambi [za kila aina], ukandamizaji bila ya haki na kumshirikisha Allaah kwa [chochote kile] ambayo hakukiteremshia mamlaka na kusema juu ya Allaah yale ambayo hamyajui.”(07:33)

Miongoni mwa maovu kwa dhati yake ni kule mtu kuzungumza juu ya kitu kwamba ni mema ilihali hajui kuwa ni mema kweli au akasema kuwa ni maovu ilihali hajui kuwa ni maovu kweli.

2 – Awe ni mwenye kujua kuwa yule anayemzungumzisha ameacha ya wajibu kwake au amefanya yaliyokatazwa. Ikiwa hajui basi haijuzu kwake kufanya hivi. Kwa sababu hapo atakuwa amezungumza juu ya asichokijua. Allaah  (Ta´ala) amesema:

وَلاَ تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْؤُولاً

“Na wala usiyafuate yale usiyokuwa nayo elimu. Hakika masikio na macho na moyo, vyote hivyo vitaulizwa.” (17:36)

Kuna watu ambao wana ghera na pupa ya kuamrisha mema na kukataza maovu wanakuwa na papara. Wanakataza pasina kujua hali ya yule mzungumzishwaji. Kwa mfano anamuona mtu yuko na mwanamke sokoni na papohapo anamvamia ni kwa nini anatembea na mwanamke. Hajui kuwa huyu ni Mahram wake, jambo ambalo ni kosa kubwa. Ukiwa na shaka linalotakiwa kwako ni kumuuliza kwanza kabla ya kuzungumza. Lakini ikiwa hakuna alama yoyote zenye kuwajibisha kumtilia mtu huyu shaka, usizungumze kitu…

3 – Kukataza kwako maovu na kuamrisha mema kusipelekei katika jambo ambalo ni ovu zaidi kuliko unalotaka kuondosha. Ikiwa hilo linapelekea katika jambo ovu zaidi kuliko unalotaka kuondosha haijuzu. Hili ni kutokana na kanuni ya kufanya maovu madogo kwa kuepusha makubwa.Tuchukulie utamuona mtu anavuta sigara lakini ukimkataza hilo litamfanya yeye kwenda na kunywa pombe. Katika hali hii hatumkatazi. Ikiwa tutajua kuwa hili litamfanya mtu huyu kwenda na kufanya lililo kubwa zaidi hhatutomkataza kuvuta sigara.

[1]Muslim (1006).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Riyaadh-is-Swaalihiyn (02/162-165)
  • Imechapishwa: 30/04/2024