Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Kukisemwa: “Ni nani Mola Wako?” Jibu: “Mola Wangu ni Allaah ambaye amenilea na akawalea walimwengu wote kwa neema Zake. 

MAELEZO

Pindi Shaykh (Rahimahu Allaah) alipobainisha misingi mitatu kwa njia ya ujumla ndipo akataka kuibainisha kwa upambanuzi mmoja baada ya mwingine kwa dalili zake kutoka katika Qur-aan na Sunnah kutoka katika alama za Allaah katika ulimwengu na kutoka katika dalili za kiakili. Hivi ndivo mtu anatakiwa kuijenga ´Aqiydah yake juu ya Qur-aan na Sunnah na kwa kutazama alama za Allaah katika ulimwengu ili ikite na ithibiti moyoni na kuondosha hoja zote.

Kuhusu ´Aqiydah zilizojengeka juu ya hoja tata, mashaka, maneno ya watu na kufuata kichwa mchunga ni ´Aqiydah zenye kuondoka ambazo hazithibiti. Ni ´Aqiydah zenye kukabiliwa na makosoaji na ubatilishwaji. ´Aqiydah haithibitishwi wala hukumu nyenginezo isipokuwa kwa dalili za Qur-aan na Sunnah na kwa dalili za akili iliyosalimika. Kwa ajili hiyo ndio maana Shaykh (Rahimahu Allaah) ametaja kwa wingi dalili juu ya misingi hii mitatu. Havuki msingi isipokuwa anautia nguvu kwa dalili na hoja za kiyakini ambazo zinaondosha mashaka na matamanio na inaifanya ´Aqiydah kuwa imara ndani ya moyo. Maneno yake (Rahimahu Allaah):

“Kukisemwa?”

Bi maana ukiulizwa ni nani Mola Wako? Hili swali limethibiti na utaulizwa nalo duniani na Aakhirah. Ni lazima kumtambua Mola Wako (´Azza wa Jall) na ujibu kwa majibu sahihi yaliyojengwa juu ya yakini na hoja. Sema:

“Mola wangu.”

Hili ndio jibu. Mola ambaye amenilea na akawalea walimwengu wote kwa neema Zake. Hii ni dalili ya kiakili.

Mola (Jalla wa ´Alaa) ni Yule ambaye anawalea waja wote kwa neema Zake, anawatunuku kwa riziki Zake na akawaumba baada ya kwamba walikuwa ni kitu kisichotajwa ndani ya tumbo za mama zao. Amemuumba umbo baada ya umbo katika viza vitatu. Anawatunuku riziki mpaka kwenye tumbo za mama zao. Kwa ajili hiyo ndio maana mtoto hukuwa mkubwa tumboni mwa mama yake. Kwa sababu anafikiwa na riziki kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na hufikiwa na chakula. Kisha anapuliziwa roho akaanza kutikisika na akapata uhai kwa idhini ya Allaah. Haya ndio malezi tumboni. Kisha anapotoka basi Allaah (Subhaanah) anamlea kwa neema Zake, kumpa afya njema, anamnywesha maziwa ya mama yake. Matokeo yake anakuwa mpaka anaanza kula chakula na anajitosheleza kutokamana na maziwa. Kisha anakuwa mkubwa hatua kwa hatua kuanzia akili yake, usikizi wake na uoni wake. Anakuwa hatua kwa hatua mpaka anafika miaka ya kubaleghe. Kisha anazidi kukuwa mpaka anafikisha miaka arobaini na anakuwa na nguvu za mwisho kabisa.

Ni nani anayempa chakula kuanzia ile siku aliyozaliwa tumboni mwa mama yake mpaka pale anapokufa? Ni nani ambaye humpa chakula? Ni nani ambaye huingiza chakula na kinywaji hichi mwilini mwake na kikaingia ndani ya kila seli, kila kiungo na kila sehemu mwilini mwake? Ni nani anayemwingizia chakula na kinywaji chake na kumwondoshea madhara yake? Ni nani ambaye huyafanya haya na akamlea mtu huyu? Je, si ni Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)? Huyu ndiye Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) anayelea, ambaye amemilia na akawalea viumbe wote kwa neema Zake. Kila kilichoko juu ya ardhi katika ulimwengu wa watu, ulimwengu wa wanyama, ulimwengu ulioko nchikavu na baharini, kuanzia viumbe vikubwa na viumbe vidogo, nchikavu na baharini, vyote vinanufaika kwa neema na riziki Yake. Amesema (Ta´ala):

أَمَّنْ هَـٰذَا الَّذِي يَرْزُقُكُمْ إِنْ أَمْسَكَ رِزْقَهُ

“Au ni nani huyu ambaye atakuruzukuni ikiwa ataizuia riziki Yake?”[1]

وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا

“Hakuna kiumbe chochote ardhini isipokuwa riziki yake iko kwa Allaah na anajua mahali pake na mapitio yake na pa kuhifadhiwa kwake.”[2]

وَكَأَيِّن مِّن دَابَّةٍ لَّا تَحْمِلُ رِزْقَهَا اللَّـهُ يَرْزُقُهَا وَإِيَّاكُمْ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

”Viumbe wangapi hawabebi riziki zao; Allaah huwaruzuku wao na nyinyi. Naye ndiye Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa kila kitu.”[3]

Huyu ndiye Mola (Subhaanah):

إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۖ مَا مِن شَفِيعٍ إِلَّا مِن بَعْدِ إِذْنِهِ ۚ ذَٰلِكُمُ اللَّـهُ رَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ

“Hakika Mola wenu ni Allaah ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita kisha akalingana juu ya ‘Arshi; Anaendesha mambo yote. Hakuna mwombezi yeyote isipokuwa baada ya idhini Yake. Huyu ndiye Allaah, Mola Wenu, hivyo basi mwabuduni.”[4]

Asiyekuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa) hamiliki katika hivyo chochote. Si masanamu wala vyenginevyo. Hakuna yeyote anayemiliki katika riziki chochote. Wao ni wenye kuruzukiwa na wameumbwa mfano wako.

[1] 67:21

[2] 11:06

[3] 29:60

[4] 10:03

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 94-97
  • Imechapishwa: 15/12/2020