42. Kumbe kitabu “Usuwl-uth-Thalaathah” kina umuhimu kiasi hichi!

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukiambiwa: “Ni misingi ipi mitatu ambayo ni wajibu kwa mtu kuijua?” sema: “Mja kumjua Mola Wake, dini yake na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

MAELEZO

Misingi – Ni wingi wa msingi. Msingi ni kile ambacho kunajengwa vyengine juu yake. Tawi ni kile kinachojengwa juu ya kingine. Hii ndio imeitwa misingi kwa sababu juu yake kunajengwa vyengine katika mambo ya dini. Kwa ajili hiyo ndio maana ikaitwa misingi kwa sababu juu yake yanajengwa mambo mengine ya dini. Dini yote inazunguka kwenye misingi hii.

Mja kumjua Mola Wake…  – Hii ndio misingi ya dini kwa ujumla na upambanuzi wake utakuja – Allaah akitaka – katika maneno ya Shaykh (Rahimahu Allaah).

Ni kwa nini misingi mitatu hii imefanywa kuwa maalum? Kwa sababu ndio misingi ya dini ya Uislamu. Jengine ni kwa sababu ndio maswali matatu anayoulizwa mtu pindi anapolazwa ndani ya kaburi. Kwa sababu mja anapolazwa ndani ya kaburi na akamwagiwa udongo na watu wakaondoka wakirejea kwa familia zao basi hujiwa na Malaika wawili ndani ya kaburi lake, roho yake ikarudishwa kwenye kiwiliwili chake, akapewa uhai wa ndani ya kaburi na sio kama uhai wa duniani. Ni uhai ambao Allaah ndiye anaujua zaidi. Watamkaza ndani ya kaburi lake na kumuuliza: “Ni nani Mola Wako? Ni ipi dini yako? Ni nani Mtume Wako?” Muumini atasema: “Mola wangu ni Allaah, dini yangu ni Uislamu na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Mtume wangu.” Ataulizwa tena: “Uliyajua vipi?” Atasema: “Nilikisoma Kitabu cha Allaah ndio nikajua.” Ataita Mwenye kuita: “Amesema kweli mja wangu, mtandikieni kitanda kutoka Peponi, mfungulieni mlango kutoka Peponi, mpanulieni kaburi lake upeo wa macho na atajiwa na harufu na upepo kutoka Peponi ambapo ataona makazi yake Peponi na aseme: “Ee Mola! Lete Qiyaamah ili niweze kurejea kwa familia na mali yangu.

Kuhusu mwenye mashaka ambaye aliishi juu ya shaka na mashaka na kutokuwa na yakini ijapokuwa alikuwa akidai Uislamu. Kama alikuwa na shaka na mashaka juu ya dini ya Allaah, kama mfano wa wanafiki, basi atababaika. Atapoambiwa: “Ni nani Mola Wako?” Atasema: “Sijui.” Atapoulizwa: “Ni ipi dini yako?” Atasema: “Sijui.” Atapoulizwa: “Ni nani Mtume wako?” Atasema: “Sijui. Aah, aah,  sijui. Niliwasikia watu wakisema kitu na mimi nikakisema. Bi maana duniani alikuwa akisema yale yanayosemwa na watu bila kuyaamini. Huu ndio mnafiki. Huu ndiye mnafiki ambaye alidhihirisha Uislamu ilihali si mwenye kuuamini ndani ya moyo wake. Alionyesha Uislamu kwa sababu ya manufaa yake ya kidunia. Duniani alikuwa mwenye kusema kwamba Mola Wake ni Allaah ilihali si mwenye kumwamini. Moyo wake unampinga. Akisema kuwa Uislamu ndio dini yake na wakati huohuo si mwenye kuamini Uislamu. Moyo wake ni wenye kupinga. Akisema kuwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye Mtume wake ilihali moyoni mwake si mwenye kuamini ujumbe wa Muhammad. Alikuwa akiyasema hayo kwa mdomo wake tu. Huyu ndiye mnafiki. Ataambiwa: “Hukujua na wala hukusoma.” Atapigwa chuma cha moto ambapo atapiga ukelele ambao lau ungelisikiwa na watu na majini basi wangelizimia. Ukelele huo unasikiwa na kila kitu isipokuwa tu watu. Watu wangeliusikia basi wangelizimia na kufa kutokana na mshtuko. Kaburi lake litambana mpaka mbavu zake zikutane, atafunguliwa mlango wa Moto na ajiwe na sumu zake na Moto wake.” Aseme: “Ee Mola! Usilete Qiyaamah. Haya ndio maisha yake na hali yake ndani ya kaburi. Hayo yote kwa sababu hakujibu majibu ya kisawasawa. Hapo ndipo ataita Mwenye kuita: “Amekadhibisha mja wangu, mtandikieni kitanda kutoka Motoni na mumfungulie mlango kutoka Motoni. Masuala haya yakishakuwa na umuhimu kama huu basi ni lazima kwetu kuyasoma na kuyaamini. Haitoshi kujifunza nayo tu. Bali tuyasome, kuyaitakidi, kuyaamini na kuyatendea kazi midhali bado tukingali hai. Huenda kwa kufanya hayo Allaah akatuthibitisha wakati tutapoulizwa ndani ya kaburi. Allaah (Ta´ala) amesema:

يُثَبِّتُ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا بِالْقَوْلِ الثَّابِتِ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَيُضِلُّ اللَّـهُ الظَّالِمِينَ ۚ وَيَفْعَلُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ

“Allaah huwathibitisha wale walioamini kwa kauli thabiti katika maisha ya duniani na Aakhirah na Allaah huwaacha kupotoka madhalimu; na Allaah anafanya akitakacho.”[1]

Misingi hii mitatu ina umuhimu mkubwa. Ndio maana Shaykh ameyatilia umuhimu katika kitabu hichi na akayaweka wazi zaidi ili tuyasome, tuyaingie ndani, tuyaamini na kuyatendea kazi. Pengine kwa kufanya hivo Allaah akatuthibitisha sote kwa kauli imara katika maisha ya duniani na Aakhirah.

[1] 14:27

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 91-94
  • Imechapishwa: 15/12/2020