Kutaka kinga ni kule kumuomba akulinde, akuzuilie na akuhifadhi. Kutaka uokozi ni kule kumuomba akuondoshee yale mazito yaliyokufika, jambo ambalo linakuwa kwa Allaah pekee ambaye ndiye muweza juu ya kila jambo.

Kutaka uokozi ni kama kutaka kinga ambapo kumekusanya ukamilifu wa kujidhalilisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuamini kuwa anatosha.

Maneno Yake (Ta´ala):

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ

“Pale mlipomuomba uokozi Mola wenu Naye akakujibuni.”[1]

Aayah hii imeteremka katika vita vikuu vya Badr. Washirikina walikuwa zaidi ya waislamu mara tatu. Waislamu, wakiongozwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), walimwelekea Allaah awanusuru na awaokoa kutokana na kisimamo hiki walichokuwemo. Imepokelewa kwamba ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Ilipokuwa siku ya Badr Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatazama Maswahabah ambao walikuwa mia tatu na kitu kidogo na akawatazama washirikina ambao walikuwa elfu na zaidi. Katika mapokezi mengine imepokelewa ya kwamba walikuwa kati ya elfu moja na mia tisa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaelekea Qiblah akiwa na shuka yake ya juu na ya kikoi chake kisha akasema:

“Ee Allaah! Nipe kile Ulichoniahidi! Ee Allaah! Nipe kile Ulichoniahidi! Ee Allaah! Ukiangamiza kikundi hiki kichache cha waislau basi hutoabudiwa ardhini.”

Akaendelea kumnong´oneza Mola wake hali ya kuwa amenyoosha mikono yake na huku ameelekea Qiblah mpaka ikaanguka shuka yake ya juu ikamporomoka kutoka mabegani mwake. Abu Bakr akamwendea na kuokota shuka yake na kuirudisha juu ya mabega yake kisha akamshika kifuani mwake na kumkumbatia na kusema: “Ee Mtume wa Allaah!  Inatosha ulivyomuomba kwa sauti Mola wako. Hakika Atakutekelezea yale aliyokuahidi.”[2]

Ndipo Allaah akateremsha Aayah hiyo.

[1] 08:09

[2] Muslim (1763).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 67
  • Imechapishwa: 12/02/2023