42. Changamoto za makafiri kwa Mtume juu ya kufufuliwa

Vivyo hivyo wanampa changamoto Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema ni lini hicho Qiyamaah?

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي ۖ لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ

”Wanakuuliza kuhusu Saa ni lini kitatokea? Sema: ”Hakika ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha wakati wake isipokuwa Yeye.”[1]

يَسْأَلُكَ النَّاسُ عَنِ السَّاعَةِ ۖ قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ

”Watu wanakuuliza kuhusu Saa. Sema: ”Ujuzi wake uko kwa Allaah.””[2]

Hakuna yeyote zaidi ya Allaah anayejua ni lini kutasimama Qiyaamah. Hajui jambo hilo si Mtume aliyetumilizwa wala Malaika aliye karibu na Allaah. Wakati Jibriyl alipomuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mbele ya Maswahabah zake: “Nieleze kuhusu Qiyaamah?” Akajibu:

“Muulizwaji si mjuzi zaidi kuliko muulizaji.”[3]

Bi maana mimi na wewe tunalingana; hatujui. Kwa sababu haya hayajui yeyote isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Jengine ni ipi faida yao wakijua ni lini kitasimama? Hawana faida yoyote katika hilo. Faida inapatikana katika kujiandaa na kufanya matendo. Lakini kuhusu ni lini Qiyaamah kitasimama ni jambo hawana faida nalo. Vinginevyo Allaah angeliwabainishia. Lakini si jengine isipokuwa ni kwa sababu ya kiburi na ukaidi. Vinginevyo ni jambo linalojulikana kwamba akikujia mtu na kukwambia unakabiliwa na adui usipojiandaa kukutana naye na kutahadhari naye basi atakuua, je, ni hekima kuanza kuuliza ni lini atakuja adui huyo? Hii sio hekima na wala busara. Hekima ni wewe kujiandaa na kufanya maandalizi mazuri pindi atapokuja. Kadhalika Qiyaamah. Hekima ni wewe kujiandaa. Kuhusu ni lini kitakuja ni jambo halina manufaa na wewe si kwa karibu na wala kwa mbali:

وَإِنْ أَدْرِي أَقَرِيبٌ أَم بَعِيدٌ مَّا تُوعَدُونَ

“Na wala sijui ni yako karibu au mbali yale mliyoahidiwa.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hajui jambo hili na wala hakuna yeyote anayejua haya isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hayo ni kutokana na hekima asiyoijua yeyote isipokuwa Yeye.

[1] 07:187

[2] 33:63

[3] al-Bukhaariy (4777) na Muslim (9,10) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Ameipokea pia Muslim (08) kupitia kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] 21:109

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 06/04/2021