41. Changamoto za makafiri kwa Allaah juu ya kufufuliwa

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Naitakidi imani kwa kile alichokhabarisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) miongoni mwa mambo yatayokupitika baada ya kifo.”

MAELEZO

Miongoni mwa nguzo za imani ni kuamini siku ya Mwisho. Ni jambo limetajwa kwa kukariri katika Qur-aan tukufu. Mwanzoni mwa Suurah “al-Baqarah” amesema (Ta´ala):

وَبِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ

“… na ni wenye yakini na Aakhirah.”[1]

Miongoni mwa sifa za wenye kumcha Allaah ni kwamba wanayakinisha siku ya Mwisho. Kuamini siku ya Mwisho ni katika wema. Amesema (Ta´ala):

وَلَـٰكِنَّ الْبِرَّ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ

“Lakini wema ni mwenye kuamini Allaah na siku ya Mwisho.”[2]

Wanamwamini Allaah na siku ya Mwisho. Ni jambo limekariri ndani ya Qur-aan tukufu. Imeitwa “siku ya Mwisho” kwa sababu ni baada ya dunia. Dunia ndio siku ya kwanza na siku ya Qiyaamah ndio siku ya Mwisho. Imeitwa “siku ya Qiyaamah” kwa sababu watu watasimama kutoka ndani ya makaburi yao mbele ya Mola wa walimwengu. Hii ni nguzo miongoni mwa nguzo za imani ambazo makafiri wengi wamekwenda kinyume nazo. Makafiri ambao walitumiliziwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa ni wenye kukufuru siku ya Mwisho:

زَعَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن لَّن يُبْعَثُوا ۚ قُلْ بَلَىٰ وَرَبِّي لَتُبْعَثُنَّ ثُمَّ لَتُنَبَّؤُنَّ بِمَا عَمِلْتُمْ ۚ وَذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

”Waliokufuru wamedai kwamba hawatofufuliwa kamwe. Sema: “Bali hapana! Naapa kwa Mola wangu! Bila shaka mtafufuliwa, kisha mtajulishwa kwa yale yote mliyoyatenda, na hayo kwa Allaah ni mepesi.”[3]

يَوْمَ يَجْمَعُكُمْ لِيَوْمِ الْجَمْعِ ۖ ذَٰلِكَ يَوْمُ التَّغَابُنِ

”Siku atakayokukusanyeni kwa ajili ya siku ya mkusanyiko.”[4]

Yule mwenye kupinga siku ya Mwisho na anapinga kufufuliwa ni mwenye kumkufuru Allaah (´Azza wa Jall). Inahusiana na ukafiri mkubwa unamtoa mtu katika Uislamu. Kwa sababu anapinga nguzo miongoni mwa nguzo za imani. Jengine anamkadhibisha Allaah na Mtume Wake. Vilevile amekadhibisha kitu kinachotambulika fika katika dini. Hawana hoja wala utata wowote zaidi ya kwamba wanaona kuwa ni jambo lisilowezekana. Kwa sababu eti wamekuwa mabaki na mifupa na wanaona ni nani awezaye kuhuisha mifupa ilihali imeshaoza na kusagika?

وَقَالُوا أَإِذَا كُنَّا عِظَامًا وَرُفَاتًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ خَلْقًا جَدِيدًا

“Wakasema: “Je, hivi sisi tukiwa mifupa na mapande yaliyosagikasagika hivi sisi hivyo tutafufuliwa katika umbo jipya?”[5]

قَالُوا أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ

“Wamesema: “Je, tutakapokufa na tukawa mchanga na mifupa, je, hivi sisi tutafufuliwa?”[6]

Na Aayah nyinginezo mfano wake.

Wanaona uwezo wa Allaah wa kuhuisha mifupa baada ya kuoza na kusagika na kuirudisha baada ya kuwa imeshakuwa udongo wanaona ni jambo liko mbali na wanasema:

قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Tuleteeni mababa zetu mkiwa nyinyi ni wakweli.”[7]

Wanampa changamoto Allaah na kusema ikiwa kweli lipo jambo la kufufuliwa baba zetu wamekwishakufa na kwamba awahuishe ilihali ni wenye kutazama jambo hilo:

قَالُوا ائْتُوا بِآبَائِنَا إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Tuleteeni mababa zetu mkiwa nyinyi ni wakweli.”

Allaah (Jalla wa ´Alaa) ameeleza kuwa hageuzi mwenendo Wake kwa sababu ya haraka za makafiri. Allaah amehukumu kwamba kufufuliwa kunakuwa katika wakati wake. Kwa hiyo haharakishi jambo hilo kwa sababu ya haraka za makafiri:

قُلِ اللَّـهُ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يَجْمَعُكُمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ لَا رَيْبَ فِيهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Sema: “Allaah anakuhuisheni, kisha atakufisheni, halafu atakukusanyeni siku ya Qiyaamah isiyo na shaka ndani yake, lakini hata hivyo watu wengi hawajui.”[8]

Allaah amehukumu kwamba kufufuliwa kuna muda wake ambao hautosogea mbele na wala hautochelewa. Hakuna yeyote awezaye kumtia presha Allaah (Jalla wa ´Alaa) na wala hageuzi ahadi na wakati Wake (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa sababu yao.

[1] 02:04

[2] 02:177

[3] 64:07

[4] 64:09

[5] 17:49

[6] 23:82

[7] 45:25

[8] 45:26

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 63-64
  • Imechapishwa: 06/04/2021